UN yajadiliana kuhusu shughuli za kulinda amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

UN yajadiliana kuhusu shughuli za kulinda amani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya mkutano kuhusu mageuzi katika shughuli za kulinda amani za umoja huo, huku Marekani ikisema itapunguza mchango wake na kuzitaka nchi wanachama kuchangia zaidi gharama zake.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley ameuambia mkutano wa baraza hilo uliofanyika chini ya mwenyekiti Mark Rutte, Waziri Mkuu wa Uholanzi, kwamba Marekani itaendelea kuwa mchangiaji mkubwa, lakini itapunguza mchango wake hadi asilimia 25 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 28.5.

''Nchi moja haipaswi kubeba mzigo wa zaidi ya robo ya bajeti ya shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na tunatarajia kuona mgawanyo sawa katika kuchangia bajeti miongoni mwa nchi wanachama. Marekani haitolipa zaidi ya asilimia 25 ya bajeti hiyo,'' alisema Haley.

Uamuzi huo umechukuliwa wakati ambapo serikali ya Rais Donald Trump inataka kupunguza kutoa misaada ya kigeni na kufanyiwa mageuzi kwa shughuli za Umoja wa Mataifa.

USA UN Botschafterin der USA Nikki Haley (picture alliance/dpa/AAM. Elshamy)

Balozi wa Marekani UN, Nikki Haley

Haley amesema hatua ya kupunguzwa kiwango hicho cha fedha iliidhinishwa mwezi Juni. Amesema Marekani itahakikisha fedha hizo zinapunguzwa kwa kuzingatia haki na busara bila kuathiri shughuli hizo.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu miongoni mwa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, bajeti ya shughuli za kulinda amani ya mwaka 2017 hadi 2018 ilipitishwa kuwa Dola bilioni 6.8, huku nchi 10 zikilipa zaidi ya nusu. Mchangiaji mkubwa wa pili katika shughuli za kulinda amani baada ya Marekani ni China ambayo inatoa asilimia 10.25 ya bajeti ikifuatiwa na Japan, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Urusi, Italia, Canada na Uhispania.

Wawakilishi wa Ulaya wametoa wito wa kuzifanya shughuli za kulinda amani kuwa za kisasa na kutovumilia kabisa unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na wanajeshi hao. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema umoja huo unaimarisha utoaji wa mafunzo kwa wanajeshi wake wa kulinda amani na unapitia upya shughuli zote za kulinda amani.

Gutteres amesema wanajeshi hao mara nyingi wanafanya kazi katika mazingira hatari, wanakabiliwa na ukosefu wa vifaa na mafunzo na wamekuwa wakilengwa katika mashambulizi na kutolea mfano kwa mwaka uliopita pekee, ambapo wanajeshi 59 wa kulinda amani waliuawa. Pia amesema wanakumbana na tofauti ya utamaduni, kamandi na udhibiti wa kijeshi.

Zentralafrikanische Republik UN Soldaten (Getty Images/AFP/P. Pabandji)

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa una vikosi 15 vya kulinda amani duniani kote. Vikiwa na zaidi ya wanajeshi 105,000, polisi pamoja na wafanyakazi wa kawaida, vikosi hivyo vinaendesha shughuli zake kuanzia Haiti hadi maeneo ya India na Pakistan. Wanajeshi wengi wako katika nchi za Afrika.

Kikosi kikubwa cha wanajeshi wa kulinda amani kiko katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambako Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekubaliana siku ya Jumanne kuongeza muda wa shughuli za kikosi hicho chenye wanajeshi 16,000 kwa mwaka mmoja zaidi.

Baadhi ya vikosi vya kulinda amani vimesifiwa kwa kuwasaidia na kuwalinda raia pamoja na kurejesha utulivu, lakini vingine vimekosolewa kwa rushwa na kukosa ufanisi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP
Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com