1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shughulli za ugavi wa nafaka kuanza tena bandari za Ukraine

Sylvia Mwehozi
28 Julai 2022

Ukraine imeanza tena operesheni za uuzaji nafaka katika miji kadhaa muhimu ya pwani. Bandari za Odesa, Chernomorsk na Pivdennyi zinatarajiwa kuanza tena usafirishaji wa nafaka kupitia bahari nyeusi.

https://p.dw.com/p/4EkUC
Ukraine Odesa | Hafen
Picha: aptyp_kok/YAY/IMAGO

Hatua hiyo inafuatia makubaliano yaliyofikiwa baina ya Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa ya kuruhusu mauzo ya nje ya nafaka. Kulingana na Ukraine, meli zilizobeba nafaka zitaanza safari kwa makundi kwa ajili ya usalama. Uturuki nayo imesema kwamba imefungua kituo cha uratibu wa pamoja kulingana na makubaliano.

Urusi iliishambulia bandari ya Odesa saa chache baada kusainiwa makubaliano na kuzidisha wasiwasi juu ya utekelezaji wake. Wakati huohuo Rais Volodomyr Zelenskyy ametangaza kuwa Ukraine itaongeza mauzo ya umeme kwa nchi za Umoja wa Ulaya wakati Urusi ikipunguza usambazaji wa gesi.

Ukraine | Antonovsky Brücke über Dnepr in Cherson
Daraja linaloelakatisha mto Dnieper Picha: Sergei Bobylev/TASS/dpa/picture alliance

Kwingineko

Afisa mmoja wa Ukraine ameeleza kuwa Urusi inabadili mbinu za mapigano na kujielekeza zaidi katika mkakati wa kujihami wakati ikifanya usambazaji mkubwa wa wanajeshi.

Oleksiy Arestovych ambaye ni mshauri kwa rais Volodomyr Zelenskyy amesema hivi sasa wanajeshi wa Urusi wanalenga kuyalinda maeneo ya kusini ambayo yanashikiliwa na Moscow badala ya kuteka maeneo mapya. Wakati afisa huyo akitoa matamshi hayo, vikosi vya Urusi vimekiteka kituo cha pili kwa ukubwa nchini Ukraine cha nishati katika mkoa wa Donetsk.

Ukraine iliweka wazi kwamba inakusudia kuudhibiti tena mji wa bandari wa kusini wa Kherson, ambao unadhibitiwa na Moscow. Hivi karibuni Kiev ililishambulia daraja muhimu ambalo linakatisha katika Mto Dnieper kwenye eneo la Kherson. Daraja hilo pia linategemewa pakubwa na Urusi katika shughuli za ugavi.