1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Urusi imeharibu kituo cha umeme Dnipro

13 Februari 2024

Maafisa wa Ukraine wamesema Urusi imeushambulia kwa makombora mji wa katikati mwa nchi hiyo wa Dnipro na kuharibu kituo kimoja cha kufua umeme pamoja na miundombinu ya usambazaji maji kwa baadhi ya wakaazi wa eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4cLgJ
Ukraine Kyiv, kombora la angani la Urusi
Uharibifu wa shambulizi la Urusi KyivPicha: Ruslan Kaniuka/Ukrinform

Kamandi ya jeshi la anga ya Ukraine imesema mji huo wenye chini ya wakaazi milioni moja ulilengwa kwa kombora na makundi manne ya droni zilizorushwa kutoka upande wa kusini, mashariki na kaskazini.

Wakati hayo yakijiri Urusi imeyaonya mataifa ya magharibi kuwa Moscow itachukua hatua nzito iwapo Marekani na Umoja wa Ulaya zitakamata mali zaidi za nchi hiyo zenye thamani ya mabilioni ya dola.

Matamshi hayo yametolewa na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi, Maria Zakharova, baada ya Umoja wa Ulaya kutia saini sheria ya kuzuia faida ya kiasi dola bilioni 300 iliyopatikana kupitia mali za benki kuu ya Urusi ilizozizuia.