1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Putin azuru mikoa miwili inayokaliwa na Urusi

Daniel Gakuba
18 Aprili 2023

Ikulu ya Urusi imearifu kuwa rais Vladimir Putin amefanya ziara katika mikoa ya Kherson na Luhansk mashariki mwa Ukraine inayokaliwa na Urusi, na alikutana na makamanda wa vikosi vya Urusi katika mikoa hiyo.

https://p.dw.com/p/4QEzM
Vita vya Ukraine| Rais wa Urusi Vladimir Putin atembelea eneo la vita mashariki mwa Ukraine
Rais wa Urusi Vladimir Putin (katikati) akiwa na makamanda wa jeshi la Urusi katika mkoa wa Kherson mashariki mwa UkrainePicha: Kremlin.ru via REUTERS

Mkanda wa vidio uliochapishwa na Kremlin umemuonyesha Rais Vladimir Putin akiwa katika mazungumzo na makamanda wa jeshi la Urusi katika makao makuu wa vikosi vinavyopigana nchini Ukraine. Mkuu wa jeshi la angani Luteni Jenerali Mikhail Teplinsky ni miongoni mwa maafisa wa ngazi ya juu waliompokea Putin, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Kremlin iliyochapishwa Jumanne, bila kueleza ziara hiyo ilifanyika lini.

Soma zaidi: Mawaziri wa G7 waahidi kuwakabili washirika wa Urusi

Ingawa hii ni mara ya pili kwa Rais Putin kutembelea maeneo ya Ukraine yanayodhibitiwa na Urusi, ni mara ya kwanza kufika katika mikoa ya Kherson na Luhansk, ambayo Urusi haiidhibiti kikamilifu. Tangazo la Kremlin limesema kuwa Putin aliwatakia wanajeshi wa Urusi sikukuu njema ya Pasaka, ambayo Wakristu wa madhehebu ya Orthodoksi waliisherehekea Jumapili iliyopita.

Vifaru vya Urusi katika mazoezi kwa makuruta wapya
Mojawapo ya vifaru vya Urusi vinavyotumiwa na makuruta wanaotayarishwa kwenda vitaniPicha: Lev Fedoseyev/Tass/dpa/picture alliance

Ukraine imeikosoa vikali ziara hiyo ya Putin, huku Mikhailo Podolyak ambaye ni mshauri wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akisema imedhihirisha kwamba uwezo wa Putin kujidhalilisha hauna kikomo.

Mapigano makali yaendelea Bakhmut

Hayo yakijiri, kamanda wa majeshi ya nchi kavu ya Ukraine Oleksandr Syrskyi amesema kupitia taarifa, kuwa mapigano makali yameendelea katika mji unaopiganiwa vikali wa Bakhmut, akiongeza kuwa Urusi inatumia ndege za kivita zinazowalenga wanajeshi wa Ukraine kwa mizinga mizito. Taarifa za hivi karibuni zinabainisha kuwa Urusi inadhibiti takribani asilimia 80 ya mji huo baada ya miezi kadhaa ya mapigano.

Soma zaidi:  Lula ahimiza upatanishi wa pamoja kumaliza mzozo nchini Ukraine

Nje ya uwanja wa vita, juhudi za kidiplomasia nazo zinaendelea. Ukraine imekaribisha leo juhudi za Brazil za kutaka kuchangia katika usuluhishi wa mzozo baina ya Ukraine na Urusi, na kuongeza kuwa bado haijauona mpango mwingine wa amani ambao shirika la habari la Bloomberg limesema kuwa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ananuia kuuwasilisha kwa China, kama msingi wa mazungumzo baina ya Urusi na Ukraine.

Luiz Inacio Lula da Silva - 100 Tage als Präsident im Amt
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, kauli yake kuwa Marekani inachochea vita vya Ukraine imeikasirisha WashingtonPicha: Eraldo Peres/AP/picture alliance

Vita vya maneno kati ya Marekani na Brazil

Wakati huo huo Marekani na Brazil zimetupiana lawama kuhusu vita hivi vya Ukraine, baada ya Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva kuituhumu Marekani kuchochea vita hivyo kwa msaada wa kijeshi inaoipatia Ukraine. Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Kirby amesema kwa kauli hiyo, Rais Lula amekariri kama kasuku propaganda ya China na Urusi, bila kujali uhalisia wa mambo.

Soma zaidi: Pasaka ya Orthodox nchini Ukraine yagubikwa na mashambulizi

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov aliyefanya ziara nchini Brazil Jumatatu wiki hii, amesifu mtazamo wa nchi hiyo mwenyeji wake, akisema imetambua kilipo chanzo cha mzozo.

 

Vyanzo: dpae, rtre, afpe