1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhalifu wa kivita Syria sasa kuchunguzwa

Sylvia Mwehozi
22 Desemba 2016

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekubaliana kuunda jopo litakalo kusanya ushahidi kuhusu uhalifu wa kivita nchini Syria ikiwa na hatua ya kuwawajibisha waliohusika na mauaji katika mgogoro wa karibu miaka sita.

https://p.dw.com/p/2UhjQ
Aleppo Evakuierung
Picha: Reuters/A. Ismail

Azimio la kuanzisha mchakato wa uchunguzi lilipitishwa na mataifa 193 kwa kura 105 zilizokubali azimio hilo,15 zikilikataa na mataifa 52 hayakuwepo. Jopo hilo linatarajiwa kufanya kazi kwa ukaribu na Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ambayo imewasilisha ripoti kadhaa zenye maelezo ya mauaji ya zaidi ya watu laki tatu yaliyotekelezwa wakati wa vita.

Mashirika ya kiraia yamekuwa yakiandaa nyaraka, orodha ya mashahidi na picha za vidio ambavyo vyote hivi vinaweza kutumiwa siku moja mahakamani kutoa ushahidi.

Urusi aliye mshirika mkuu wa Syria pamoja na China mwaka 2014 walipinga ombi la baraza hilo kuwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ianze uchunguzi wa makosa ya jinai nchini Syria.

Azimio hilo lililondaliwa na Liechtenstein kwa ushirikiano na mataifa 58 yakiwemo Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Ujerumani pamoja na nchi za Uturuki, Saudi Arabia na Qatar.

UN Sicherheitsrat in New York zur Lage in Syrien, Aleppo
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jijini New YorkPicha: Getty Images/D. Angerer

Akilihutubia baraza hilo, balozi wa Liechtenstein Christina Wenaweser amesema azimio hilo litahakikisha wahusika wanawajibishwa . Nikimnukuu anasema kuwa" hatimaye tunachukua hatua ya maana kufikia matarajio ambayo tuliyashindwa kwa muda mrefu" mwisho wa kunukuu.

Balozi wa Syria Bashar Jafaari amekosoa hatua hiyo akisema inakwenda kinyume na mkataba wa Umoja wa Mataifa na ni uingiliaji wa masuala ya ndani wa taifa mwanachama wa Umoja huo.

Urusi, China na Iran ni miongoni mwa mataifa yaliyolipinga azimio hilo linalompatia majukumu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuripoti ndani ya siku 20 ya kuanzishwa kwa jopo jipya litakalofadhiliwa na Umoja wa Mataifa.

Jopo litakusanya, kuhifadhi na kuchambua ushahidi wa ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya utu na haki za binadamu pamoja na ukandamizaji mwingine na kuandaa nyaraka zitazoharakisha na kuwezesha mchakato wa mashitaka ya jinai.

Syrien Avakuierung aus Aleppo
Mama akiwa na watoto wake baada ya kuondolewa AleppoPicha: Getty Images/AFP/B. Al-Halabi

Hayo yakijiri mjini Aleppo kwenyewe, zoezi la kuwaondoa raia na waasi limeendelea jana Jumatano baada ya kusimama kwa siku moja. Farhan Haq ni naibu msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na amesisitiza juu ya ulinzi wa raia kama jambo muhimu linalofuatiliwa. "Raia wote waliosalia lazima waruhusiwe kuondoka salama ikiwa watachagua kufanya hivyo. Kuwapatia misaada wenye uhitaji, kuwaokoa na misaada ya kiutu ni jambo pia linalohitajika." amemalizia msemaji huyo.

Serikali ya Syria ilikuwa imesema zoezi hilo limekamilika wakati jeshi likijiandaa kuuchukua mji huo lakini Umoja wa Mataifa na waasi wamekanusha taarifa hizo, wakisema zoezi lingali bado linaendelea.

Raia wameshuhudiwa wakipigwa na baridi kali wakati wakiyasubiria mabasi yaliyokwama mjini Aleppo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Zainab Aziz