1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yaishutumu Uturuki kuchochea mivutano Mediterenia

12 Oktoba 2020

Ugiriki imeishutumu Uturuki kuchochea mivutano mashariki mwa bahari ya Meditterania kufuatia tangazo la Uturuki kuwa itatuma meli ya utafiti kwa ajili ya mpango maalum wa kufanya utafiti katia eneo hilo linalozozaniwa.

https://p.dw.com/p/3jnBn
Greek PM Mitsotakis meets with Politburo member of the Communist Party of China and director of the Central Foreign Affairs Commission Office Yang Jiechi
Picha: REUTERS

Uturuki jana Jumapili ilitangaza kwamba meli yake ya utafiti itabakia katika eneo hilo hadi October 22 na ujumbe huo ulitumwa kuelekea,NAVTEX ambao ni mfumo wa kufuatilia tahadhari ya safari za baharini.

Ugiriki leo kupitia wizara yake ya mamo ya nje imeonesha kughadhabishwa na kitendo hicho cha Uturuki na kusema kwamba wanaitaka nchi hiyo kuufuta mara moja uamuzi wake huo, na kuongeza kusema kwamba utafiti huo mpya wa Uturuki utasababisha mgogoro mkubwa na kitisho cha moja kwa moja kwa amani na usalama wa kanda hiyo.

Meli ya utafiti ya kituruki ya Oruc Reis iliyoondoka leo kwenye bandari ya Antalya, itakwenda karibu na kisiwa cha Ugiriki cha Kastellorizo kama sehemu ya operesheni hiyo na itafuatiwa na meli mbili nyingine za nchi hiyo Ataman na Cengiz Han.

Meli ya Oruc Reis ilirudi pwani ya Uturuki

Mivutano kati ya Uturuki na Ugiriki iliongezeka mnamo mwezi Agostibaada ya meli ya utafiti wa uchimbaji gesi kuingia eneo hilo la bahari ya Meditterania linalozozaniwa upande wa Mashariki ikisindikizwa na meli za kivita. Uturuki ilidai kwamba meli hiyo ilikuwa kwenye harakati ya utafiti wa shughuli za kijiolojia , na hatua hiyo ilikosolewa vikali na Umoja wa Ulaya na Ugiriki.

Türkei - Forschungsschiff
Meli ya Uturuk ya Oruc ReisPicha: Orhan Cicek/AA/picture-alliance

Meli ya Oruc Reis ilirudi kwenye pwani ya Uturuki mwezi uliopita katika kile kilichoonekana kuwa unaweza kuwa mwisho wa mgogoro huo wa kisiasa.

Rais wa Uturuki wakati huo alisema kwamba ilikuwa ni hatua ya kutowa fursa kwa mchakato wa kidiplomasia lakini maafisa wa Uturuki walisema ni hatua iliyochukuliwa ili meli hiyo ifanyiwe matengenezo yaliyopangwa na kwamba meli hiyo itarejea kwenye eneo hilo la bahari.

Na kama haitoshi matumaini ya kupunguza mivutano yalifufuliwa tena wakati nchi zote mbili zilipokubaliana na mpango uliofikiwa kwa usimamizi wa jumuiya ya kujihami ya NATO wa kuanza tena mdahalo kuhusu mvutano huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas atakwenda uturuki

Na wiki iliyopita,mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote mbili Uturuki na Ugirikiwalikutana pembezoni mwa jukwaa la usalama lililofanyika katika mji mkuu wa Slovakia,Bratislava. Na mazungumzo hayo ndiyo yaliyokuwa ya ngazi ya juu tangu ulipoanza mgogoro huu.

Deutschland I Fragestunde BT - Heiko Maas -  Bundesregierung
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: Uwe Koch/Eibner-Pressefoto/picture-alliance

Lakini hatua ya sasa ya Uturuki kupeleka meli yake ya Utafiti mara tu baada ya hatua zote hizo kupigwa inaonesha Uturuki haiwezi kuaminika na haitaki mazungumzo ,hivyo ndivyo inavyosema wizara ya mambo ya nje ya Ugiriki.

Kimsingi waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amepangiwa kwenda Uturuki siku ya Jumatano kwa mujibu wa shirika la habari la Uturuki TRT. Na suala hilo la mgogoro wa kuwania eneo la bahari mashariki mwa Meditterania huenda likawa ajenda kuu .

Ikumbukwe kwamba Hatua ya Uturuki ya kuipeleka tena Meli yake ya utafiti kwenye eneo hili imekuja siku moja baada ya wizara yake ya mambo ya nje kutoa tamko linaloishutumu Ugiriki kwa kutokuwa mkweli kutokana kile ambacho Uturuki inakiona kuwa vitendo vya kuongeza mvutano wakati Ugiriki ikijitangaza kuwa tayari kwa mazungumzo.