1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yawarejesha raia waliodanganywa ajira Thailand

24 Mei 2024

Uganda imewarejesha nyumbani raia wake 23 waliokuwa wamepelekwa nchini Myanmar baada ya kuhadaiwa kwamba wangepata kazi za malipo ya juu katika nchi jirani ya Thailand.

https://p.dw.com/p/4gFXe
Bitcoin
Bitcoin, mojawapo ya sarafu za mtandaoni.Picha: Cigdem Simsek/Zoonar/picture alliance

Habari za raia hao na wengine ambao bado wamekwama katika nchi hizo mbili zilianza kusambaa mwishoni mwa mwaka 2023.

Kulingana na watu hao waliopokelewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe siku ya Alhamisi (Mei 23), walipofika Thailand walitoroshwa hadi Myanmar na kuhusishwa katika kashfa za utakatishaji wa sarafu za mtandaoni.

Fahamu zaidi kuhusu sarafu za kidijitali

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nje ya Uganda, Vincent Bagiire, aliyewapokea rasmi watu hao uwanjani hapo, alielezea kuwa waliokuwa wamewateka watu hao walitaka kulipwa pesa za kikombozi kabla ya kuwaachia.

"Imechukuwa zaidi ya miezi minne kuwashawishi wawaachie raia hawa tukisaidiwa na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) pamoja na serikali za Thailand na Myanmar," alisema Bagiire.

Sema Uvume: Sarafu mpya ya mtandaoni ya WorldCoin

Kufuatia masaibu hayo, wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo imewataka raia wake na wengine kutoka Afrika kuchukuwa tahadhari dhidi ya ahadi za kazi na kwenda bila kupata hakikisho kutoka serikali zao.

Kulingana na Balozi wa Uganda nchini Malaysia,  Betty Bigombe, ambaye alihusika moja kwa moja kuwakomboa watu hao, kuna zaidi ya Waafrika 100,000 ambao wamekwama katika nchi hizo mbili baada ya kutoroshwa.