Uchaguzi wa Bunge la Ulaya Ireland na Jamhuri ya Cheki | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya Ireland na Jamhuri ya Cheki

Wapiga kura wa Ireland na Jamhuri ya Czech wanalichagua bunge la Ulaya. Nchini Ireland uchaguzi huo unafanyika katika hali ya taharuki kufuatia mpango wa Brexit, uliomlazimisha Waziri Mkuu Theresa May kujiuzulu.

 

Kasheshe ya Brexit inafuatiliziwa kwa makini zaidi na wakaazi wa Ireland ambao Uingereza ndio mshirika wao wa karibu zaidi wa kibiashara, ikihifia kurejeshwa mpaka pamoja na  jimbo la Uingereza la Ireland ya Kaskazini.

Vituo vya kupiga kura vimefunguliwa tangu saa moja za asubuhi na vyama vingi vya nchi hiyo vimepania kuhakikisha wanaendelea kubakia wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Katika jamhuri ya Tcheki, nchi pekee ambako zoezi la uchaguzi litaendelea kwa siku mbili, vituo vya kupiga kura vitafunguliwa saa nane za mchana na kesho vitafunguliwa saa mbili za asubuhi. Chama cha siasa kali kinachoongozwa na waziri mkuu, bilioneya Andrej Babis kinatarajiwa kushinda licha ya maandamano dhidi ya serikalai ya nchi hiyo iliyojiunga na Umoja wa ulaya tangu mwaka 2004.

Makundi ya kizalendo na  yale ya siasa kali za mrengo wa kulia yanatarajiwa kufanya vyema katika uchaguzi huo huku makundi mawili muhimu katika bunge la Ulaya, wahafidhina wa EPP na wasocial Democrat - PSE wakipoteza kura.

Frans Timmermans wa chama cha Labour cha uholanzi azusha maajabu

Frans Timmermans wa chama cha Labour cha uholanzi azusha maajabu

Uholanzi imezusha maajabu

Hata hivyo nchini Uholanzi ambako wapiga kura waliteremka vituoni jana, chama cha Labour cha Frans Timmermans , mshika bendera wa kundi la vyama vya kijamaa katika bunge la Ulaya EPP, anaetaka kugombea wadhifa utakaoachwa na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker kimezusha maajabu kwa kuibuka na ushindi bila ya kutarajiwa. Kwa mujibu wa matokeo ya awali chama hicho cha Labour cha Uholanzi kimejikingia zaidi ya asili mia 18.1 ya kura na kuwaacha nyuma wafuasi wa chama cha kihafidhina cha waziri mkuu Mark Rutte na kile cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachoongozwa na Thierry Baudet.

Waingereza na waholanzi ndio waliokuwa wa mwanzo kupiga kura jana. Kesho itakuwa zamu ya Lithuania, Malta na Slovakia na nchi zilizosalia za Umoja wa Ulaya zitapiga kura jumapili inayokuja.

Zaidi ya wapiga kura milioni 400 kutoka nchi 28 wanatakiwa wakaatoe sauti zao kuwachagua wabunge 751 wa Ulaya. Matokeo rasmi yatatangazwa jumapili usiku, vituo vya kupigia kura vitakapofungwa katika nchi zote wanachama.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef