Uchaguzi wa Brandenburg na Saxony wakodolewa macho Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Uchaguzi huu ni mtihani kwa serikali kuu ya mseto

Uchaguzi wa Brandenburg na Saxony wakodolewa macho Ujerumani

Ni uchaguzi unaofuatiliwa kwa karibu Ujerumani kuona nani ataibuka mwenye nguvu kati ya wenye siasa kali na vyama vikuu vilivyozoeleka. Chama cha siasa kali kinachopinga wageni AfD kinapewa nafasi kubwa Brandenburg.

Majimbo ya Ujerumani ya  Brandenburg na Saxony yanafanya uchaguzi leo Septemba Mosi na matokeo ya uchunguzi wa maoni tayari yalishaonesha kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa chama cha siasa kali kisichopendelea wageni kinachoitwa chama mbadala kwa Ujerumani (AfD).

Chama hicho kinatarajia kupata uungwaji mkono Jumapili hii katika uchaguzi huo unaofanyika katika majimbo hayo mawili ambayo zamani yalikuwa ya kikomunisti. Mbali na chama cha AfD kujitangaza kwa kuupinga Uislamu na wanaotaka hifadhi ya ukimbizi,chama hicho kimejijenga pia umaarufu kutokana na suala la kuzungumzia pengo la utajiri lililopo kati ya Mashariki na Magharibi tangu kuanguka ukuta wa Berlin mwaka 1989.

Hisia za chuki zinazokuzwa na AfD

Kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa kikitumia msemo uliokuwa ukitumika zamani na wapigania Demokrasia unaosema ''Sisi ndio watu'' na kuugeuza kuwa fimbo dhidi ya kile walichokipa jina kuwa ''Utawala wa Merkel. Ikumbukwe kwamba Ujerumani Mashariki ni nyumbani kwa viongozi wengi wa AfD wenye msimamo mkali zaidi miongoni mwao akiwemo Bjoern Hoecke ambaye ameiita makumbusho ya mauaji ya Holocoust mjini Berlin kuwa sanamu la fedheha.

 Rafiki yake wa karibu Andreas Kalbitz mwenye umri wa miaka 46 aliyewahi kuwa mwanajeshi wa kuruka na mwamvuli ambaye amekuwa na ukaribu mkubwa na makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia,ndiye mgombea mwenye nafasi kubwa katika jimbo la Brandenburg.

Jarida la kila wiki la Der Speigel liliripoti kwamba mwaka 2007 Kalbitz alijiunga na kundi linalojulikana nchini Ujerumani la wanazi mambo leo alipokuwa ziarani mjini Athens Ugiriki na kuja kugundulika kwa polisi kutokana na bendera ya Manazi ya nembo ya Swastika iliyokuwa ikipeperushwa katika Balkoni ya Hoteli.

Kalbitz alilithibitisha jarida hilo kwamba alijiunga kwenye ziara hiyo lakini akasisitiza kwamba  shughuli iliyofanyika haikuwa katika mazingira ya kumshawishi zaidi kimaslahi au kumuidhinisha. Katika jimbo la Brandenburg chama cha AfD kinachuana kwa karibu sana na chama kinacholiongoza jimbo hilo kwa sasa cha Social Democratic SPD,ambapo vyama vyote vina zaidi ya asilimia 20.

Katika Jimbo la Saxony ambako ndiko liliko asisiwa kundi la siasa kali linalochukia waislamu la Pegisa,chama cha AfD kimepoteza kidogo umaarufu kikiachwa nyuma na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Kansela Angela Merkel,Christian Democratic Union,CDU.

Ushindi usiokuwa na tija

Hata hivyo,ikiwa chama cha AfD kitapata viti vingi na kuibuka kuwa chama chenye nguvu katika jimbo lolote kati ya hayo mawili,vyama vingine vikubwa vinatarajiwa kujiweka kando na chama hicho na kukizuia kuongoza serikali,kwa kuunda muungano ili kupata wiki mkubwa unaohitajika.

Kwa maana hiyo, mtaalamu wa sayansi ya siasa Wolfgang Schroeder kutoka chuo kikuu cha Kassel anasema kujipatia ushindi wa viti vingi huenda kukaonesha tu mafanikio yasiyokuwa na tija kwa AfD. Na kwa upande mwingine kushindwa katika uchaguzi kwa chama cha CDU au mshirika wake mdogo serikali ya SPD kutasababisha kitisho kingine katika muungano unaoyumbayumba.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri. Tatu Karema

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com