1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi ulioahirishwa Nigeria kufanyika Jumamosi

Admin.WagnerD22 Februari 2019

Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari amewahimiza raia wa nchi hiyo kujitokeza kesho Jumamosi na kupiga kura katika uchaguzi wa rais na bunge ulioahirishwa na tume ya uchaguzi kwa juma moja akiahidi usalama utakuwa wa kutosha.

https://p.dw.com/p/3Dqmd
Nigeria - Wahl verschoben
Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Akilihutubia taifa mkesha wa uchaguzi huo ulioahirishwa na tume ya uchaguzi kutoka Jumamosi iliyopita hadi Jumamosi ya Kesho tarehe 23 Februari, Rais Buhari amewataka Wanigeria kuweka kando mashaka na wasiwasi na kuwa na imani kuwa tume huru ya kitaifa ya uchaguzi INEC itaendesha vyema uchaguzi huo.

Rais huyo wa Nigeria anayekabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mfanyabiashara tajiri Atiku Abubakar ameendelea kusema raia hawapaswi kuwa na wasiwasi kutokana na uvumi kuwa kutakuwa na ghasia kwani asasi za kiusalama zimeweka hatua za kutosha za kiusalama.

Buhari mwenye umri wa miaka 76, anagombea awamu ya pili madarakani kuendelea kuliongoza taifa hilo imara zaidi barani Afrika na lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani humo likiwa na takriban watu milioni 200 lakini masuala ya usalama kusuasua kwa uchumi, ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana na ufisadi yamempunguzia umaarufu kwani Wanigeria wanamshutumu kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake za kuyashughulikia hayo katika awamu yake ya kwanza madarakani.

Boko Haram yatoa vitisho

Mutmaßlicher Boko-Haram-Angriff in Nigeria
Picha: picture-alliance/AP/Jossy Ola

Kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limefanya mashambulizi kadhaa katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno, limewaonya raia dhidi ya kushiriki katika uchaguzi huo wa kesho.

Atiku Abubakar, makamu wa rais wa zamani wa Nigeria ambaye anakiongoza chama kikuu cha upinzani cha People's Democratic Party PDP, kupitia ukurasa wa Twitter pia amewatolea wito wapiga kura kujitokeza kwa wingi ili kuwachagua viongozii watakaoifanya Nigeria kuimarika tena na kulinda kura zao.

Abubakar mwenye umri wa miaka 72, amesema anatumai kuwepo ushindi kama wa mwaka 2015 ambapo upinzani kwa mara ya kwanza katika historia ya Nigeria ulimshinda rais aliye madarakani.

Pande hasimu zatuhumiana

Nigeria - Wahlkampf
Picha: Getty Images/AFP/L. Tato

Pande zote mbili za kisiasa Chama cha All Progressive Congress, APC cha Buhari, na cha upinzani cha Peoples Democratic, PDP vimekuwa vikishtumiana vikali kuwa vimehusika katika kucheleweshwa kwa uchaguzi na  kula njama na tume ya uchaguzi ili kuchakachua matokeo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Mahmood Yakoob amesisitiza kuwa uchaguzi mkuu utakafanyika Jumamosi hii, akilaumu matatizo ya kiufundi kuwa sababu za kuchelewesha uchaguzi wa tarehe 16 Februari na kukanusha kuwa ilitokana na shinikizo la kisiasa.

Zaidi ya watu milioni 84 wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi huo wa rais na bunge wa hapo kesho. Uchaguzi wa kuwachagua magavana na madiwani wapya utafanyika tarehe 9 mwezi Machi.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga