1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Wademocrat wakosa muafaka wa kuifungua serikali

Daniel Gakuba
3 Januari 2019

Mkutano wa jana kati ya Rais Donald Trump na wakuu wa vyama bungeni, kujaribu kuutanzua mgogoro uliolazimisha shughuli za serikali ya Marekani kufungwa, umeambulia patupu, kila upande uking'ang'ania msimamo wake.

https://p.dw.com/p/3AwyP
USA Präsident Trump
Picha: Getty Images/Z. Gibson

Wakati mkwamo huo ukiingia siku ya 12, mambo yatachukua sura mpya leo (Alhamis), pale wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watakapofanya kikao cha kwanza mwaka 2019, chini ya udhibiti wa chama cha Democratic.

Hakuna upande ulioonekana kutetereka katika msimamo wake kuhusiana na  bajeti inayotakiwa na Rais Donald Trump ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka baina ya Marekani na Mexico. Rais Trump amesema atakaidi kuitia saini bajeti yoyote hadi pale matakwa yake ya dola bilioni 5 za kujenga ukuta huo yatakaporidhiwa, na mtu anayetarajiwa kuchaguliwa baadaye leo kuwa spika wa baraza la wawakilishi, Nancy Pelosi, amesema hata ikichukua muda gani, hawatakubali masharti hayo ya Trump.

Katika mahojiano na shirika la habari la NBC la nchini Marekani, Bi Pelosi amesema haijarishi muda itaochuwa, wala mara watakazoulizwa, jibu litabakia kuwa hapana kwa ujenzi wa ukuta. Trump naye akizungumza katika baraza lake la mawaziri ameapa kwamba msimamo wake utabaki pale pale.

Pande zote zatupiana lawama

Kila upande unajipa moyo kwamba wamarekani wanaulaumu upande mwingine kwa mkwamo huu, ambao umelemaza shughuli za wizara nane, na kuwalazimisha wafanyakazi laki nane ama kubaki nyumbani, au kufanya kazi bila malipo. Haya ni maoni ya Chuck Schumer, kiongozi wa Wademocrat walio wachache katika baraza la Seneti.

Mexiko -USA | Hugs No Walls: Familienangehörige können sich während einer kurzen Grenzöffnung umarmen
Ujenzi wa ukuta kwenye mpaka baina ya Marekani na Mexico ni ahadi muhimu ya kampeni ya Rais Trump.Picha: Getty Images/AFP/H. Martinez

''Wameanza kuwakiwa na moto. Haimsaidii rais, na haikisaidii chama cha Republican kuwajibika kuzifunga shughuli za serikali,'' amesema Schumer, na kuongeza kuwa ''tumewapa fursa ya kutoka katika hali hiyo wakati tukijadili usalama wa mpakani.''

''Kusema kwamba hatasaini bajeti na atatumia kufungwa kwa serikali kutushinikiza kusalimu amri, hilo Wamarekani hawalitaki.'' Ameongeza Chuck Schumer.

Trump hataki 'kuonekana mjinga'

Kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico ilikuwa ahadi muhimu ya kampeni ya Rais Trump, na kulingana na afisa mmoja wa Ikulu ya White House aliyenukuliwa na shirika la habari la Associted Press, amethibitisha kuwa Trump alitamka katika kikao na viongozi wa vyama, kwamba hawezi kuachana na azma ya kuujenga ukuta huo, kwa sababu akifanya hivyo ataonekana mjinga.

Wakati Trump akitaka bajeti mpya ijumuishe dola bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta, wademocrat wameridhia dola bilioni 1.3 za kuimarisha usalama kwenye mpaka huo. Warepublican wanaothibiti baraza la seneti wanasita kuikubali bajeti hiyo ya wapinzani wao, wakijua Trump ataitupilia mbali. Kiongozi wa Warepublican katika baraza hilo Mitch McConnell, amesema mvutano uliopo ni ''janga tupu.''

Baada ya mazungumzo hayo yaliyokwama, Rais Trump amesema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa twitter, kwamba bado anayo nia ya kushirikiana na Wademocrat kupata suluhisho.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, rtre

Mhariri: Grace Kabogo