1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuwapa bunduki waalimu

Saumu Mwasimba
22 Februari 2018

Wanafunzi na wazazi waililia serikali nchini Marekani kwa kushindwa kudhibiti bunduki wakati nchi hiyo ikishuhudia mara kwa mara mashambulizi ya ufyetuaji risasi mashuleni

https://p.dw.com/p/2t84I
USA Washington - Trump trifft auf Überlebende des Amoklaufs der Douglas High School in Florida
Trump akizungumza na walionusurika shule ya Florida na wazazi waoPicha: picture-alliance/abaca/D. Olivier

Rais Donald Trump amewaambia wanafunzi walionusurika katika mashambulizi ya ufyetuaji risasi katika shule ya Florida pamoja na jamaa zao kwamba atafikiria hatua ya kuwapa walimu bunduki. Kadhalika rais huyo ameahidi kuanzisha utaratibu wa uchunguzi wa afya ya akili pamoja na umri kwa watu wanaonunua bunduki.

Marekani inakabiliwa na maandamano ya wanafunzi  dhidi ya serikali kushindwa kuchukua hatua ya kudhibiti bunduki katika wakati ambapo nchi hiyo imekuwa ikishuhudia mara kwa mara mashambulizi ya risasi katika shule kadhaa. Wakati wanafunzi wakifanya maandamano hayo rais Donald Trump alichukua fursa hiyo hapo jana katika mkutano unaojadili suala hilo la vurugu za kutumia bunduki kuunga mkono fikra ya kuwapa mafunzo ya kutumia silaha walimu pamoja na wafanyakazi wengine katika juhudi za kuzuia vurugu hizo za kutumia bunduki mashuleni.

Mkutano wa jumatano  umekuja ikiwa ni wiki moja baada ya mtu aliyekuwa na bunduki kufyetulia risasi kiholela na kuuwa watu 17 katika shule moja ya sekondari huko Florida.Trump amesema kwamba anafikiria kuunga mkono mapendekezo yaliyotolewa ya kuruhusu ubebaji wa bastola ndogo ambazo zitawawezesha wafanyakazi fulani wa shule kuwa katika nafasi ya kujibu mashambulizi pale inapotokea dharura.Kwa mtazamo wa rais huyo wa Marekani pendekezo hilo huenda likasuluhisha tatizo kwa kuwafanya washambuliaji kufikiri mara mbili. Hata hivyo wanafunzi waliokuwa wakiandamana wanaikosoa serikali inavyolishughulikia suala la kudhibiti bunduki.

USA Washington - Trump trifft auf Überlebende des Amoklaufs der Douglas High School in Florida
Mwanafunzi aliyenusurika mashambulizi ya shule ya Florida akumbatiwa na mmoja wa wazaziPicha: Reuters/J. Ernst

''kila mwaka unaoingia unajua tu kwamba kutakuwepo na mashambulizi mengine ya risasi,kutakuwa na wahanga wengi sana,wako wengi watakaolia. Kwahivyo muda wowote ninapokuwa shule ninajawa na khofu na kufikiria kwamba je ikiwa hii ndio itakayokuwa mara yangu ya mwisho,je ikiwa hii ndiyo itakayokuwa mara ya mwisho kuwaona wazazi wangu''

Wanafunzi chungunzima walijitokeza nje ya ikulu ya Marekani Washington Dc jana jumatano wakiishinikiza serikali kuweka sheria ya kudhibiti bunduki. Maandamano hayo yalikuwa ni sehemu ya harakati za nchi nzima zilizoanzishwa na wanafunzi wa shule za sekondari kufuatia mauaji ya wiki iliyopita yaliyosababishwa na mshambuliaji aliyewafyetulia watu risasi katika shule ya sekondari ya Marjory Stoneman Douglas,Parkalnd Florida.

Kwa upande wake rais Trump amesisitiza mwito wake wa kufanyanyika ukaguzi mkali kwa watu wanaonunua bunduki huku akitilia zaidi mkazo juu ya suala la watu kuangalia taarifa zao za kiafya kuhusu ugonjwa wa akili na pia umri huku akisisitiza kwamba mara hii suala hilo halitozungumzwa tu kwa maneno matupu bali kwa vitendo. Hata hivyo chama cha wafanyibiashara wa bunduki nchini Marekani kimelalamika kikisema kwamba juhudi za kuongeza kigezo cha umri kwa wanunuzi wa bunduki pamoja na bastola kitawanyima vijana wakimarekani  haki yao ya kujilinda. Kulikuweko na hamaki iliyoonekana waziwazi kutoka kwa wazazi waliohudhuria mkutano huo waliomtaka rais Trump kulishughulikia suala hilo kwa uthabiti mkubwa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/DW Web

Mhariri: Josephat Charo