Trump: Katiba haitoi haki ya uraia kwa kuzaliwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.10.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump: Katiba haitoi haki ya uraia kwa kuzaliwa

Rais wa Marekani Donald Trump amesema katiba ya nchi hiyo haikikishi haki ya uraia kwa kila mmoja anaezaliwa nchini humo, na kwamba ataendeleza shinikizo lake kukomesha utaratibu huo.

Trump ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Jumatatu kwamba kile kinachoitwa haki ya uraia wa kuzaliwa, ambacho kinaigahrimu Marekani mabilioni ya dola na kinawanyima haki raia wa Marekani, kitakomeshwa kwa njia moja ama nyingine.

Ameongeza kuwa suala hilo halikuzingatiwa katika marekebisho ya 14 ya katiba kwa sababu ya kuwekewa masharti, na kumalizia kwamba wataalamu wengi wa sheria wanakubalina na hilo.

Kipengele hicho cha 14, kilichoongezwa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani, kinatoa uraia kwa yeyote aliezaliwa katika ardhi ya Marekani, na kilinuwiwa kutoa ulinzi wa kikatiba kwa watumwa wa zamani.

Lakini wanasiasa wa Republican kama vile Trump wanasema kinaweka mazingira kwa watu kuingia nchini humo kinyume cha sheria na kuzaa watoto.

Wakili ambaye ni mume wa mmoja wa washauri wa juu wa Trump, Kellyanne Conway, aliandika kwenye makala ya maoni leo kwamba hatua kama hiyo ya kukomesha haki ya uraia wa kuzaliwa itakuwa inakiuka katiba.

Mexiko - Migranten aus Mittelamerika auf dem Weg in die USA - in San Pedro Tapanatepec (Getty Images/AFP/G. Arias)

Wahamiaji kutoka Amerika ya Kati waliopo kwenye msafara unaokwenda Marekani kutafuta aisha bora. Trump ameapa kupambana na uhamiaji haramu.

Kutumia amri ya rais kufuta sheria

Rais Trump alisema mjini Axios kwamba atatoa amri ya rais kufuta kipengele kinachowapa watoto wa wageni na wahamiaji wasioruhusiwa, haki ya kuwa raia.

Msemaji wa ikulu ya White House Sarah Sanders amesema katika mahojiano na kito cha televisheni cha Fox News kwamba kuna zaidi ya fumbo moja kuhusu uhamiaji.

"Kuna wataalamu kadhaa wa sheria wanaodhani kwamba kuna mambo mengi huko chini, lakini suala kubwa hapa tunalopaswa kulitazama ni sababu ya kuwa katika msimamo huu kwanza," alisema Sanders.

Amesema sababu ya hayo ni kushindwa kwa Wademocrat bungeni kusaidia kurekebisha mmfumo wa uhamiaji uliovinjika, na kwamba rais anaagalia njia zote, na "atafanya uamuzi hatimaye kuhusu njia bora ya kuhakikisha usalama wa mipaka yetu na kusimamia sheria na utaratibu nchini mwetu."

Utawala wa Trump umewaweka kizuwizini maelfu ya wahamiaji haramu chini ya sheria ya uhamiaji ya Marekani, kwa madai kwamba hawaingii katika mamlaka ya kisheria ya Marekani.

Trump pia ametangaza kuwa anapeleka wanajeshi zaidi ya 5000 kuimarisha ulinzi kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, kuzuwia msafara wa wahamiaji kutoka America ya Kati wanaoelekea nchini humo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com