1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atumia hotuba ya kukubali uteuzi kumshambulia Biden

Mohammed Khelef
28 Agosti 2020

Rais Donald Trump wa Marekani anayetetea kiti chake alitumia hotuba yake ya kukubali uteuzi wa chama chake cha Republican kumshambulia zaidi mpinzani wake mkuu, makamo rais wa zamani Joe Biden, akimuita msoshalisti.

https://p.dw.com/p/3hdFa
USA Nominierungsparteitag der Republikaner | Donald Trump
Picha: Imago Images/UPI/K. Dietsch

Ingawa amekosolewa kwa kutumia Ikulu ya White House, ambayo ni miliki ya serikali, kufanyia shughuli za chama chake, Trump alihutubia mkutano mkuu wa Republican kukubali uteuzi wa kutetea wadhifa wake, akiwa kwenye ikulu hiyo, ambapo sehemu kubwa ya hotuba hiyo ilikuwa ni mashambulizi dhidi ya hasimu wake, Biden, akirejea shutuma zake kuwa ni msoshalisti anayetaka kuiangamiza Marekani.

"Licha ya utukufu wetu wote kama taifa, kila tulichofanikiwa sasa kinahatarishwa. Huu ni uchaguzi muhimu kabisa kwenye historia ya nchi yetu. Wapigakura hawajawahi kukabiliwa na chaguo la wazi baina ya vyama viwili, dira mbili, falsafa mbili, ama ajenda mbili kama mara hii. Uchaguzi huu utaamuwa ama tunaiokowa Ndoto ya Marekani, au ikiwa tunaruhusu ajenda ya kisoshalisti kuuharibu mustakbali wetu," alisema Trump huku akishangiriwa mara kwa mara ya wageni wake.

Katika wakati ambapo Marekani imeshapoteza zaidi ya watu 180,000 kutokana na janga la virusi vya korona, Trump alitoa hotuba yake mbele ya kadamnasi ya watu zaidi ya 1,000 waliosimama mbele ya bendera za Marekani na huku wakipiga mayowe ya "Miaka Minne Mingine" na "U.S.A.!"

Kuhusu suala hilo la COVID-19, Trump alimkosoa Biden aliyesema atasikiliza ushauri wa kisayansi kuhusiana na janga la korona, hata ikibidi kuweka marufuku ya nchi nzima, akisema makamo huyo wa zamani wa rais "si mwokozi bali mtu aliyejisalimisha mbele ya korona."

Ghasia na machafuko ya kibaguzi

	USA Nominierungsparteitag der Republikaner
Mkutano wa Trump kukubali uteuzi wa chama chake kutetea nafasi ya urais kwenye uchaguzi wa Novemba 2020.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Lugha yake ilikuwa ni mwangwi wa hotuba yake kama huo kwenye mkutano wa mwaka 2016, ambao pia ulifanyika wakati nchi ikiwa kwenye mpasuko mkubwa wa ubaguzi wa rangi, baada ya maafisa wanane wa polisi kuuawa katika miji ya Texas na Louisiana kufuatia maandamano na ghasia zilizosababishwa na mauaji ya polisi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. 

Lakini Trump aliyewania kwa mafanikio akiwa mkando miaka minne iliyopita, sasa ndiye anayeidhibiti Ikulu ya  White House, jambo lililompa nguvu kwenye kauli yake kwamba ni yeye tu anayeweza kulitatuwa tatizo hilo la ghasia zinazotokana na ubaguzi wa rangi, ambazo anadai zimeshamiri kwenye miji inayotawaliwa na mahasimu wake wa Democratic.

"Hatutakiwi kuruhusu utawala wa kihuni. Hatuwezi kuuruhusu utawala huo wa kihuni. Kwa nguvu kabisa, chama cha Republican kinalaani ghasia, wizi, uchomaji moto na machafuko tuliyoyaona kwenye miji inayotawaliwa na Democratic kama Kenosha, Minneapolis, Porland, Chicago na New York. Kuna hatari na ghasia kwenye miji mingi inayoongozwa na Democrat kote Marekani. Tatizo hilo linaweza kutatuliwa na sisi kama wakituita. Tuiteni tu. Tuko tayari kuja."

Kama ishara ya namna Marekani ilivyogawika, waliohudhuria mkutano huo waliweza kusikia kelele za waandamanaji wakipiga honi karibu na jengo la White House, wakati Trump akihutubia.