Trump amteua Mattis kuwa waziri wa ulinzi | NRS-Import | DW | 02.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Trump amteua Mattis kuwa waziri wa ulinzi

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump ametangaza kumteua aliyekuwa Jenerali wa Jeshi la Wanamaji, James Mattis, kuwa waziri wa ulinzi. Hata hivyo uteuzi huo utahitaji idhini maalumu kutoka Baraza la Gongress la Marekani.

Trump alitangaza uamuzi huo katika mkutano wa kwanza wa hadhara tokea kumalizika kwa kampeni za uchaguzi, uliofanyika mjini Cincinnati jimbo la Ohio.

"Tutamteua Mad Dog Mattis kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani. Lakini tangazo rasmi litatolewa Jumatatu kwa hiyo usimwambie mtu yeyeto. Mad Dog. Ni mtu mashuhuri sana," amesema Donald Trump.

Jenerali huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 66, na anayejulikana kwa jina la utani la 'Mad Dog' lenye maana ya mbwa mwenye kichaa, alistaafu mwaka 2013 baada ya kuwa mkuu wa makao makuu ya vikosi vya ulinzi Marekani akiwa na mamlaka juu ya vikosi vilivyokuwa Iraq na Afghanistan pamoja na jukumu la kusimamia eneo linalojumuisha nchi kadhaa zikiwamo Syria, Yemen na Iran.

Lakini chini ya sheria za Marekani za hivi sasa, hatoruhusiwa kuongoza wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, hadi itimie miaka saba tokea kumaliza kazi ya kijeshi.

Congress kupiga kura ya kubatilisha sheria hiyo

Kwa maana hiyo, baraza la Congress litahitaji kupiga kura ya kubatilisha sheria hiyo, iliyopo kuhakikisha jeshi la Marekani linadhibitiwa na kiongozi wa kiraia.

 General James Mattis (Getty Images for DIRECTV/B. Steffy)

Aliyekuwa Jenerali wa jeshi la wanamaji, James Mattis

Kwa mujibu wa historia ya Marekani, wabunge waliwahi kufanya hivyo mara moja tu tokea kuundwa sheria hiyo miaka 65 iliyopita. Mnamo mwaka 1950 wabunge wa Marekani walimpigia kura ya aina hiyo Jenerali George Marshall, ambaye alikuwa Mkuu wa Jeshi la Marekani wakati wa uongozi wa Rais Franklin Roosevelt pamoja na Harry Truman na ndiye aliyehusika na mpango mkubwa wa kupanua jeshi la Marekani katika historia ya nchi hiyo. Alistaafu mnamo mwaka 1945.

Tayari seneta mmoja wa chama cha Democrat, Kirsten Gillibrand, ameashiri kuwa atapinga kubatilishwa kwa sheria hiyo. Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba udhibiti wa kiraia wa jeshi la Marekani ni moja wapo ya kanuni za kimsingi za demokrasia ya nchi ya taifa hilo.

Iwapo ataidhinishwa na bunge la Congress na kuweza kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, uteuzi wa Mattis unaweza kurejesha nyuma sera ya Rais aliye madarakani kwa sasa Barack Obama kuhusu Iran. Mattis aliachishwa kazi wakati wa uongozi wa Obama, baada ya kushindwa kukubaliana na uwongozi huo juu ya namna ya kuendesha uhusiano wake na Iran.

Mattis amenukuliwa akielezea Iran kuwa ni taifa linaloendelea kuwa kitisho cha kupatikana amani na utulivu Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/rtre

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com