Trump ajitenga na sera ya ′Mataifa mawili′ kuhusu Mashariki ya Kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump ajitenga na sera ya 'Mataifa mawili' kuhusu Mashariki ya Kati

Rais Donald Trump ameipa kisogo sera ya nchi yake kuhusu amani ya Mashariki ya Kati ya mataifa mawili; Israel na Palestina. Wakati huo huo, aliyependekezwa na Rais Trump katika nafasi ya waziri wa kazi, amejiengua.

USA Israel | Benjamin Netanjahu bei Donald Trump in Washington (Getty Images/A. Wong)

Netanyahu na Trump mjini Washington

Kauli mbalimbali zilizotolewa na Rais Trump baada ya kuzungumza na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel Jumatano mjini Washington, ziliashiria kujitenga mbali na sera zilizoshikiliwa na tawala za Marekani zilizotangulia, kuhusu eneo la Mashariki ya kati. Trump alisema kwake suluhisho lolote litakuwa sawa, mradi likubaliwe na wahusika.

''Natafakari mataifa mawili, au taifa moja, na napenda chaguo linalopendwa na pande zote. Nafurahia linalopendwa na pande zote, moja au jingine.'' amesema Rais Trump akisimama kandoni mwa Netanyahu.

Mabadiliko haya ya sera ya Marekani yamefanyika kumfurahisha Netanyaho na mfungano wa vyama vya serikali ya mrengo mkali wa kulia unaounda serikali yake. Akikariri maneno ya Waziri Mkuu wa Israel, Rais Trump amesema anadhani wapalestina wanapaswa kuacha kuwapa watoto wao mafundisho ya chuki dhidi ya Israel, ambayo amesema wanayapata tangu wakiwa wachanga.

Netanyahu aweka masharti yake kwa amani

Infografik Siedlungen im Westjordanland ENGLISCH

Kielelezo cha makazi ya walowezi wa kiyahudi yaliyojengwa katika Ukingo wa Magharibi

Kwa upande wake, Netanyahu ameumwagia maneno ya sifa ushirika kati ya Israel na Marekani, na kutoa mashariti yake ya kuwepo kwa amani Mashariki ya Kati. Amesema kwanza lazima wapalestina waitambue Israel kama Taifa la Kiyahudi, na kuacha miito ya kuiangamiza nchi hiyo, na pia kutambua haki ya Israel kusimamia usalama katika eneo zima.

Amesema, ''Katika makubaliano yoyote ya amani, Israel lazima iwe na uwezo wa kudhibiti usalama katika eneo lote magharibi mwa mto Jordan, tofauti na hali hiyo, tunajua kitakachotokea.''

Eneo hilo la Ukingo wa Magharibi, ni kitovu cha taifa la Palestina linalotarajiwa, kulingana na makubaliano yote ya awali ya kimataifa.

Kuhusu suala la Makazi ya walowezi, Rais Trump amemuomba Netanyahu kujizuia kidogo, akisema anayo matumaini kuwa makubaliano yatafikiwa.

pande mbali mbali zimepinga msimamo huo mpya wa Marekani. Kiongozi wa mazungumzo kwa upande wa Palestina Saeb Erakat, amesema kauli kutoka Washington ni jaribio la kuuwa na kuzika ndoto ya wapalestina ya kuwa na taifa lao wenyewe. Umoja wa Mataifa umesema unaendelea kutambua suluhisho la mataifa mawili, kwa dhati zaidi kuliko wakati wowote ule. Na mkuu wa kamati ya bunge la Ujerumani kuhusu uhusiano wa kimataifa Norbert Roettgen, amesema mataifa mawili ndio suluhisho pekee linalowezekana katika mzozo wa Mashariki ya Kati.

Mteuliwa wa Trump kwa uwaziri wa kazi ajiengua

Wakati huo huo nchini Marekani, Mtu aliyependekezwa na Rais Donald Trump katika wadhfa wa Waziri wa Kazi, Andrew Puzder  amejiondoa katika uteuzi huo. Puzder ameichukuwa hatua hiyo baada ya wasiwasi uliokuwa ukiongezeka dhidi yake, kuhusiana na tuhuma kwamba hakulipa kodi ya mtumishi wa nyumbani kwake ambaye alikuwa hana kibali cha kufanya kazi nchini Marekani.

Uteuzi wa mtu huyo tajiri mmiliki wa mikahawa ulikuwa umeleta utata miongoni mwa wademokrat kutokana na msimamo wake  jju ya malipo ya muda wa ziada kazini na pia kiwango cha chini cha mshahara. Katika tangazo lake kupitia shirika la habari la Associated Press, Puzder amesema ataendelea kuunga mkono utawala wa Rais Donald Trump, na amethibitisha kuwa uchunguzi wa bunge kuhusu uteuzi wake ungeanza leo Alhamis.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,dpae, ape

Mhariri: Zainab Aziz

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com