1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya washushiwa hadhi ya kidiplomasia Marekani

Josephat Charo
8 Januari 2019

Utawala wa rais Donald Trump umeishusha hadhi ya kidiplomasia ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Marekani. Afisa wa Umoja wa Ulaya amethibitisha taarifa hizo kwa shirika la utangazaji la Ujerumani, DW.

https://p.dw.com/p/3BAwA
USA Haushaltsstreit in Washington - Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Hatua hiyo ya wizara ya mambo ya ndani ya Marekani ambayo haikutangazwa, na ambayo haijawahi kuripotiwa, iliishusha hadhi ya kidiplomasia ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Washington kutoka nchi mwanachama hadi shirika la kimataifa. "Hatufahamu hasa lini walipochukua hatua hiyo, kwa sababu walisahau kutuarifu," afisa mmoja anayeifahamu vizuri kadhia hiyo ameiambia DW katika mahojiano maalumu. Ninaweza kuthibitisha uamuzi huu haujapokelewa vyema mjini Brussels," akasema afisa huyo na kuongeza kwamba suala hilo na jibu rasmi la Umoja wa Ulaya bado vinajadiliwa.

Baada ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya kutambua kwamba balozi wake mjini Washington hakualikwa kuhudhuria matukio muhimu mwishoni mwa mwaka uliopita, maafisa walioandaa mazishi ya rais wa zamani wa Marekani, George H.W Bush, walitoa thibitisho la mwisho kwa wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya kwamba hadhi ya uwakilishi ilikuwa imeshushwa. Wanadiplomasia wanaamini hatua hiyo ilianza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi wa Oktoba au mapema Novemba.

Afisa wa Umoja wa Ulaya amesema, katika tukio hilo la Desemba 5, wakati wanadiplomasia walipokuwa wakikusanyika mjini Washington kutoa heshima zao, balozi wa Umoja wa Ulaya mjini Washington, David O'Sullivan, hakuitwa katika hali ya kawaida ya kufuata orodha ya mabalozi kuanzia waliohudumu kwa muda mrefu hadi wale waliohudumu kwa kipindi kifupi. Badala yake aliitwa kama mtu wa mwisho kabisa katika orodha hiyo.

Kabla ya kushushwa hadhi, O'Sullivan, ambaye amehudumu kama balozi wa Umoja wa Ulaya mjini Washington tangu mwaka 2014, angekuwa miongoni mwa mabalozi 20 au 30 kati ya wajumbe zaidi ya 150 wa kigeni wanaohudumu katika mji mkuu huo wa Marekani.

'Walisahau kutufahamisha'

Mwanadiplomasia mmoja wa nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya mjini Washington pia amethibitisha kushushiwa hadhi ya kidiplomasia umoja huo. Ameilaani vikali hatua hiyo akisema "Hili bila shaka si suala la itifaki, bali ni kitu ambacho kina nia ya wazi ya kisiasa." Mwanadiplomasia huyo aliongeza kusema kushushwa hadhi ujumbe wa Umoja wa Ulaya kumeibua mtizamo hasi na huo ndio msimamo wa idadi kubwa ya mataifa wanachama wa umoja huo.

NATO Gipel in Brüssel
Mike Pompeo, Waziri wa mambo ya nje ya MarekaniPicha: Reuters/Y. Herman

Baada ya kugundua uamuzi wa kushushwa hadhi, wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya mjini Washington waliwasiliana na wizara ya mambo ya nje ya Marekani yenye dhamana na masuala ya kidiplomasia kutafuta ufafanuzi. Afisa wa Umoja wa Ulaya alisema na hapa tunanukuu, "Walitwambia walisahau kutujulisha na kwamba huu ni uamuzi waliouchukua kwa sababu mkuu wa itifaki anafikiri ni jambo sahihi la kufanya." mwisho wa kunukuu.

Afisa huyo pia alisema hadhi ya kibalozi ya Umoja wa Ulaya mjini Washington ilipandishwa hadi ngazi ya balozi wa nchi mnamo Septemba mwaka 2016, baada ya mchakato mrefu na mgumu ulioratibiwa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani chini ya utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Barack Obama.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeshikilia msimamo wake. Katika hotuba muhimu kuhusu sera ya kigeni mjini Brussels mapema Desemba 2018, waziri wa mambo ya nchi za kigeni, Mike Pompeo, alimpongeza Trump na kuzitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuimarisha uhuru wao, sambamba na umoja huo.

Mwandishi: Josephat Charo/https://www.dw.com

Mhariri: Caro Robi