Trump aanza ziara yake rasmi ya China
13 Mei 2026
Trump aliondoka Washington jana Jumanne na akasema anatarajia mazungumzo "marefu" na Xi Jinping kuhusiana na Iran, ambayo inaitegemea China kama mteja wake mkuu wa mafuta yake yaliyowekewa vikwazo na Marekani.
Kiongozi huyo wa Marekani lakini amesema kuwa hatohitaji usaidizi wowote wa China kwa Iran.
Trump amesema pia kuwa atazungumza na Xi kuhusu Marekani kuiuzia silaha Taiwan, kisiwa chenye utawala wa ndani ambacho China inadai kuwa ni sehemu ya himaya yake.
Hatua hii itakuwa ni kinyume cha utamaduni wa kihistoria wa Marekani wa kutojadiliana na China kuhusiana na kukiunga mkono kisiwa hicho.
Wakuu hao wa nchi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani pia wanatarajiwa kujadiliana kuhusu uhusiano wao wa kibiashara na udhibiti wa China wa uuzaji wa madini muhimu yaliyo nadra.