1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May yaomba muda zaidi kwa Brexit

Daniel Gakuba
5 Aprili 2019

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ameutumia barua Umoja wa Ulaya, akiomba mchakato wa nchi yake kuondoka katika umoja urefushiwe muda hadi Juni 30. Baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo zimesema barua hiyo haitoshi.

https://p.dw.com/p/3GMu2
Rede Theresa May zu Brexit-Aufschub
Picha: Getty Images/J. Taylor

Katika barua hiyo ya waziri mkuu Theresa May, ambayo ofisi ya rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk imethibitisha kuipokea leo Ijumaa, Bi May ametaka mchakato wa nchi yake kuondoka katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit uongezewe muda wa hadi mwishoni mwa mwezi Juni, akiahidi Uingereza itaondoka kabla ya muda huo ikiwa mpango uliofikiwa kati yake na Umoja wa Ulaya utaridhiwa na bunge.

Aidha, waziri mkuu huyo amebainisha kuwa ikiwa nchi yake haitaondoka kabla ya tarehe 23 May, hapo itabidi ijiandaye kushiriki katika uchaguzi wa bunge la Ulaya, akisisitiza kwamba kwake suala lenye kipaumbele ni Uingereza kumaliza uanachama wake kupitia mpango maalumu wa ushirikiano wa baadaye.

London: Unterhaus stimmt über die Verschiebung des Brexit ab
Bunge la Uingereza limekataa mapendekezo yote ya mipango ya kuondoka katika Umoja wa UlayaPicha: Reuters TV

Awali, Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk alikuwa amependekeza Uingereza ipatiwa muda mrefu zaidi wa hadi mwaka moja, ili wanasiasa wake wanaovutana kuhusu Brexit waweze kukubaliana juu ya mpango wa talaka na Umoja na Ulaya.

Pingamizi kutoka baadhi ya nchi

Hata hivyo, kurefushwa muda huo kwa kipindi chochote kutahitaji kukubaliwa kwa kauli moja na nchi 27 zinazosalia katika Umoja wa Ulaya, na tayari baadhi ya nchi hizo zimeanza kuonyesha mashaka. Ufaransa imesema Uingereza inatakiwa kutoa ufafanuzi juu ya namna itakavyoutumia muda huo wa ziada, kabla ya kukubaliwa.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema lazima Uingereza ielewe majukumu yake sambamba na kurefushiwa muda.

Donald Tusk At European Council
Donald Tusk, Rais wa Baraza la UlayaPicha: picture-alliance/NurPhoto/N. Economou

Amesema, ''Kwa maoni yetu, ni muhimu kwamba waziri mkuu wa Uingereza aelewe kwamba kwa kurefushiwa muda hadi Juni 30, Uingereza italazimika kushiriki katika uchaguzi wa bunge la ulaya.'' na kuongeza kuwa hawezi kutabiri kitakachoamuliwa katika kikao cha Baraza la Ulaya Jumatano ijayo.

''Baraza hilo litatafakari kwa kina mapendekezo yaliyoletwa  katika barua ya waziri mkuu May.'' amesisitiza Seibert.

Malumbano ya wanasiasa ndio kikwazo

Tayari, Uingereza ambayo ingekuwa imeondoka ndani ya Umoja wa Ulaya tarehe 29 mwezi uliopita wa Machi, imekwishaongezewa muda kufikia Aprili 12, lakini bado malumbano katika bunge na ndani ya chama chake cha Conservative ycha waziri mkuu May yamezuia kupatikana mwafaka wowote kuhusu namna ya kusonga mbele.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jeremy Hunt amesema nchi yake haipendelei kurefushwa kwa muda wa brexit kusiko na ukomo, ila ameziomba nchi zinazosalia ndani ya Umoja wa Ulaya kuelewa kuwa Uingereza ni nchi yenye kufuata demokrasia, inayokumbana na changamoto ya kuwa na bunge lililoshindwa kuafikiana juu ya uamuzi wowote.

rtre, ape