Syria yazidisha kiburi | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Syria yazidisha kiburi

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid Al-Muallem amesema hakutakuwa na suluhu ya mgogoro unaoendelea nchini humo hadi pale mataifa ya kigeni yatakapoacha kuwafadhili waasi ambao serikali yake inawaita magaidi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al-Muallem akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al-Muallem akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Akionekana kutotetereshwa na matamshi makali kutoka kwa viongozi mbalimbali waliyolaani mauaji yanayoendela nchini humo, Waziri Muallem ambaye alikuwa anauhutubia Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema rais Assad yuko tayari kufanya mageuzi endapo vurugu zitasitishwa na kuongeza kuwa ili hilo lifikiwe, ipo haja kwa Umoja wa mataifa kuyashinikiza mataifa aliyoyataja kuacha kuwahifadhi, kuwapatia silaha na fedha, na kuwapa mafunzo magaidi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al-Muallem akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al-Muallem akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Muallem alizinyooshea kidole Marekani, Ufaransa, Uturuki, Qatar na Saudi Arabia kwa kuwafadhili waasi hao na kuongeza kuwa matatizo ya nchi yatatuliwa tu kwa masanduku ya kupigia kura, ingawa kwa miongo minne iliyopita, Syria ilikuwa ikiongozwa na familia ya Assad bila kuendesha uchaguzi huru na wa haki.

"Napenda kuwaambia kuwa mafanikio ya jitihada za kimataifa yanahitaji, pamoja na dhamira ya serikali ya Syria, kuyalaazimisha mataifa yanayosaidia makundi yenye silaha nchini mwangu, hususani Uturuki, Saudi Arabia, Qatar, Libya na mengine, kuacha kuyapa silaha, fedha, mafunzo na kuyahifadhi makundi ya kigaidi yenye silaha na badala yake wahamasishe majadiliano na kuacha vurugu," alisema waziri huyo.

Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa bila suluhu ya Syria

Pamoja na hotuba kadhaa, mikutano na mazungumzo ya siri, vita hivyo vinavyoendelea nchini Syria vilibaki bila kupatiwa ufumbuzi katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka huu. Wakati mkutano huo ulipofikia tamati siku ya Jumatatu, hakukuwa na mafanikio yoyote kuhusu vita hivyo, jambo lililozua maswali mapya juu ya umuhimu wa chombo hicho.

Wanawake wa Syria wanaopambana na utawala wa Syria.

Wanawake wa Syria wanaopambana na utawala wa Syria.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon aliitahadharisha Syria dhidi ya matumizi ya silaha za kemikali na kuonya kuwa shambulio lolote la namna hiyo litakuwa na madhara makubwa. Ban aliwambia waandishi wa habari katika mkutano wa kumbukumbu ya miaka 15 ya mkataba wa silaha za kemikali uliofanyika kandoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa, kuwa matumizi ya silaha hizo litakuwa kosa lisilovumilika, na kuonmgeza kuwa silaha za kemikali hazina tena nafasi katika karne ya 21. Alisema Syria na mataifa mengine saba yalikuwa hayaridhia mkataba huo.

Iran nayo yaionya Syria kuhusu silaha za kemikali

Mshirika wa karibu wa Syria, Iran nayo iliongeza sauti yake dhidi ya matumizi ya silaha za kemikali na utawala wa Syria katika mapambano yake na waasi. Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Ali Akbar Saleh, alisema mjini New York kuwa Iran haitaunga mkono nchi yoyote, ikiwemo Syria, ambayo inatumia silaha hizo na kusema huo ndiyo utakuwa mwisho wa kila kitu. Iran imekuwa ikibanwa na jumuiya ya kimatifa kwa madai ya kutaka kutengeneza silaha za nyuklia lakini inakanusha tuhuma hizo nan inaseme mpango wake wa nyuklia ni kwa matumizi tu ya kiraia.

Jinsi Mkoa wa Aleppo unapoonekana kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka vikosi vya serikali.

Jinsi Mkoa wa Aleppo unapoonekana kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka vikosi vya serikali.

Wakati huo huo, vurugu zilitokea kati ya vikosi vya usalama na wakimbizi wa Syria kaskazini mwa Jordan baada ya wakimbizi kufanya fujo wakipinga hali mbaya katika kambi pekee ya wakimbizi kutoka Syria. Kwa mujibu wa vyombo vya usalama vya Jordan, polisi wa kutuliza ghasia walipambana na wakaazi wa kampbi ya Zaatari iliyoko Mafraq baada ya wakimbizi kuanza kuichomoto kambi hiyo.

Na kutoka mjini Damascus, shirika la uangalizi wa haki za binaadamu limesema waasi wamevamia kituo cha kijeshi katika eneo la Douma lililoko kaskazini mashariki mwa mji huo na kuua wanajeshi sita, huku mashambulizi mfululizo kutoka vikosi vya serikali yakiwalaazimu kukimbia hovyo kunusuru maisha yao. Kwa mujibu shirika hilo, watu wasiyo pungua elfu 30 wameuawa tangu kuanza kwa mgogoro huo mwezi Machi mwaka jana.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, dpae,ap
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com