1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yachukuwa udhibiti wa mali zilizoidia kundi la Hamas

Tatu Karema
23 Septemba 2021

Mamlaka nchini Sudan imechukuwa udhibiti wa mali ambazo zimetumika kulisaidia kundi la Hamas kutoka Palestina, uamuzi unaoonekana kuwa sehemu ya hatua ya taifa hilo la Afrika kurejesha mahusiano yake na Israel

https://p.dw.com/p/40jyM
Sudan Neuer Premierminister Abdalla Hamdok
Picha: Reuters/M. Nureldin Abdallah

Kwa mujibu wa kikosi kilichopewa jina la Kamati ya Kuvunjilia Mbali Utawala wa Juni 30, 1989 na kurejesha fedha za umma lililobuniwa mahsusi kabisa kwa kuvunja uongozi wa Bashir, mali hiyo inajumuisha nyumba, hisa za kampuni, hoteli katika eneo moja la kifahari mjini  Khartoum, kampuni ya ubadilishanaji fedha za kigeni, kituo cha televisheni na zaidi ya ekari milioni moja za mashamba.

Afisa mmoja wa kikosi hicho amesema kuwa uwekezaji wa kundi la Hamas nchini Sudan ulianza katika biashara ndogo kama vile hoteli ndogo kabla ya kuingilia ujenzi wa nyumba. Mali zilizochukuliwa zilizoelezewa na duru rasmi ya serikali ya Sudan pamoja na duru za kijasusi za Magharibi, zinaonesha ukubwa  wa mtandao huo wa wanamgambo. Wadgi Salih, kiongozi wa kikosi hicho, amesema taifa hilo liligeuka kuwa kitovu cha utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi na kuongeza kuwa mtandao huo ulikuwa mkubwa ndani na nje ya taifa hilo.

Katar Doha | Früherer sudanesischer Präsident | Omar Hassan al-Baschir
Omar al-Bashir - Aliyekuwa rais wa SudanPicha: Photoshot/picture alliance

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wa Sudan na Palestina, wanasema kuwa kundi hilo la Hamas limepoteza uwezo wake katika mataifa ya kigeni, ambapo wanachama na wafuasi wa kundi hilo wangeweza kuishi, kukusanya pesa na kupeleka silaha na pesa katika Ukanda wa Gaza. Hata hivyo, shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa afisa wa kundi hilo Sami Abu Zuhri amekanusha kuwa kundi hilo lilikuwa na uwekezaji nchini Sudan, lakini alikubali kuweko kwa athari inayotokana na mabadiliko ya kisiasa nchini humo na kuongeza inasikitisha kwamba kulikuwa na mikakati kadhaa iliyodhoofisha uwepo wa kundi hilo nchini Sudan na kusababisha kuwepo kwa uhusiano mdogo wa kisiasa na taifa hilo.

Mbinu zilizotumika Sudan

Duru za kijasusi za Magharibi zinasema kuwa mbinu zilizotumika nchini Sudan ni za kawaida kwa uhalifu wa kupangwa: Kampuni ziliongozwa na wadhamini wa hisa, ushuru unaokusanywa kwa pesa taslimu na uhamishaji wa pesa kupitia kwa kampuni ya kubadilisha pesa za kigeni. Pamoja na kuakisi hatua ya Sudan kurejesha mahusiano ya kawaida na Israel, kutwaliwa kwa kampuni kadhaa ambazo maafisa wa serikali ya Sudan wanasema zilihusishwa na kundi la Hamas kumesaidia kuharakisha Sudan kuingiliana tena na mataifa ya Magharibi tangu kupinduliwa kwa Bashir mnamo 2019. Katika muda wa mwaka mmoja uliopita, Sudan imefanikiwa kuondolewa katika orodha ya Marekani ya wafadhili wa ugaidi na iko katika harakati ya kupata msaada wa deni la zaidi ya dola bilioni 50.