1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiChina

Starmer azuru China kurekebisha uhusiano na kupanua fursa

29 Januari 2026

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer yuko nchini China kwa ziara ya siku nne ambayo lengo lake ni kurekebisha uhusiano na kupanua fursa kwa makampuni ya Uingereza katika nchi hiyo ya pili kubwa kiuchumi duniani.

https://p.dw.com/p/57eNu
China Peking 2026 | Waziri Mkuu Keir Starmer azuru China
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer akikaribishwa katika ziara yake nchini China Januari 28, 2026Picha: Carl Court/AFP

Waziri Mkuu Keir Starmer aliwasili Beijing Jumatano kwa ziara hiyo ya kihistoria, akisaka kuimarisha kile alichokielezea kama "ushirikiano wa kivitendo" na taifa hilo lenye uchumi mkubwa kabisa barani Asia, baada ya miaka kadhaa ya uhusiano ulioyumba.

Ofisi ya Starmer ya Downing imeandika kupitia mtandao wa X kwamba, kama ishara ya mataifa hayo kufanya kazi pamoja, Alhamisi yanatarajia kusaini makubaliano ya kushirikiana katika kukabiliana na magenge yanayojihusisha na usafirishaji wa wahamiaji haramu.

Suala la uhamiaji holela ni nyeti mno kwa kiongozi huyo wa chama cha Labour ambaye tayari aliahidi kuwachukulia hatua kali walanguzi hao na kuzuia wimbi la wahamiaji wanaoingia Uingereza ambalo linachochea kuimarika zaidi kwa siasa za mrengo mkali wa kulia.

Magenge ya kusafirisha wahamiaji haramu kudhibitiwa kwa ushirikiano

Mwaka uliopita, karibu wahamiaji 42,000 waliingia Uingereza kupitia pwani yake ya kusini, wakitokea Ufaransa. Kulingana na taarifa ya Downing Street, injini za boti nyingi zinazotumiwa na magenge hayo yanayowavusha wahamiaji kupitia ujia wa English Channel hutengenezwa China.

Ufaransa Gravelines 2025 | Wahamiaji wakivuka kwenye English Channel kwa mashua
Wahamiaji hutumia mashua ndogo wanapovuka English Channel kwenye ufuo wa Gravelines, kaskazini mwa Ufaransa. Picha: Marcin Nowak/London News Pictures/ZUMA/picture alliance

Starmer atakutana kwa mazungumzo ya kama dakika 40 na Rais Xi Jinping kabla ya kupata chakula cha mchana baadae leo, lakini pia atazungumza na Waziri Mkuu Li Qiang na mbunge mwandamizi wa China Zhao Leji.

Makubaliano yatakayosainiwa yatajumuisha ushirikiano wa taarifa za kiintelijensia na mawasiliano ya moja kwa moja na wazalishaji wa vifaa vya boti wa China ili kuhakikisha kwamba hawaingizwi kwenye uhalifu wa kupanga, taarifa ya Downing Street imeongeza.

Jana Jumatano, Starmer aliuambia ujumbe aliiongozana nao wa karibu viongozi 60 wa wafanyabiashara pamoja na wawakilishi wa kitamaduni kwamba ushirikiano na China ni muhimu kwa maslahi ya kitaifa na kuwatolea wito kutumia nafasi hiyo kunufaika na fursa zitakazopatikana nchini China.

Starmer na Labour wahaha kusaka fursa za kiuchumi kwa washirika wapya

Starmer ambaye serikali yake inapambana kufanikisha ahadi yake ya kuimarisha uchumi, ametoa kipaumbele katika kuimarisha ushirikiano na China akiwa na matumaini ya kupata fursa zaidi za kibiashara.

Uswisi Davos 2026 | Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia
Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney akitoa hotuba kwenye Kongamano la Kiuchumi la Dunia, Davos - UswisiPicha: Sean Kilpatrick/The Canadian Press/AP Photo/picture alliance

Starmer anakuwa miongoni mwa msururu wa viongozi wa mataifa ya magharibi kuzuru Beijing katika wiki za karibuni, katika kile kinachoonekana kama ni kusaka washirika wapya, mbali na Marekani.

Kiongozi huyo amepitisha sera mpya kuhusu ushirikiano na China baada ya kudhoofika kwa muda mrefu chini ya serikali za kihafidhina, wakati London ilipozuia uwekezaji wa China nchini mwake kutokana na hofu ya usalama wa taifa na wasiwasi kuhusiana na ukandamizaji dhidi ya uhuru wa kisiasa huko Hong Kong.

Uingereza imejikuta kwenye mvutano na mshirika wake wa karibu Donald Trump kufuatia azma yake ya kukinyakua kisiwa cha Greenland pamoja na kitisho cha muda mfupi cha kuiweka ushuru sambamba na mataifa wanachama wa Jumuiya ya NATO, kutokana na kupinga azma yake hiyo.