1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Ukraine kusitisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo

Admin.WagnerD18 Juni 2014

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema leo kuwa ataagiza kusitishwa kwa mapigano ya upande mmoja hivi karibuni katika eneo la mashariki mwa nchi yake kama sehemu ya mpango makhususi wa kumaliza uasi wa majuma kumi

https://p.dw.com/p/1CL1Q
Picha: picture-alliance/dpa

Tangazo la Rais Poroshenko linakuja baada ya mazungumzo kati yake na Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa njia ya simu hapo jana ambapo viongozi hao wawili walizungumzia juu ya suluhisho la muda mrefu kukabiliana na uasi uliozuka mashariki mwa Ukraine tangu mwezi Aprili.

Taarifa kutoka ofisi ya Rais wa Ukraine imesema marais hao wawili walijadili masuala kadha wa kadha ya hatua zinazopaswa kupewa kipaumbele ili kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano na njia muafaka ya kulifuatilia hilo.

Mpango wa Poroshenko wa kutafuta amani nchini mwake unataka kukomeshwa kwa uhasama,waasi kupata muda wa kuweka silaha chini na Putin kutambua rasmi uongozi mpya wa Ukraine ambao uliingia madarakani baada ya kuondolewa ule uliokuwa ukiungwa mkono na Urusi mwezi Februari mwaka huu.

Poroshenko atangaza mpango makhususi wa amani

Mbali na serikali kutangaza kuwa itachukua hatua hiyo ya kusitisha mapambano dhidi ya waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa Ukraine ambao utatekelezwa kwa muda mfupi, pia mpango huo wa amani unatarajiwa kutoa msamaha kwa waasi na kuifanyia katiba marekebisho ili kulipa eneo hilo mamlaka zaidi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: picture-alliance/dpa

Poroshenko ambaye pia alizungumza na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel hakufafanua hasa ni lini mpango huo utaanza kutekelezwa.

Katika hatua nyingine iliyochukuliwa leo na Poroshenko, amempendekeza balozi wa Ukraine nchini Ujerumani Pavlo Klimkin kuwa waziri mpya wa mambo ya nchi za kigeni.

Kimkin mwenye umri wa miaka 47 iwapo ataidhinishwa na bunge atachukua wadhifa huo kutoka kwa Andry Deschychtsia.Klimkin amechangia kwa kiasi kikubwa katika mazungumzo ya kuboresha uhusiano kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya.

Rais huyo wa Ukraine pie amependekeza kuondolewa kwa gavana wa benki kuu Stephan Kubiv kama sehemu ya mbadiliko anayotaka katika serikali yake mpya.

Bomba la mafuta lashambuliwa

Wakati huo huo waziri mkuu wa Ukraine Arseny Yatsenyuk ameagiza usalama kuimarishwa katika vituo vya mabomba ya kusafirishaia gesi ili kuzuia hujuma baada ya waziri wa mambo ya ndani kusema mripuko ulitokea katika bomba moja hapo jana ulisababishwa na bomu.

Mripuko wa bomu katika bomba la gesi Ukraine
Mripuko wa bomu katika bomba la gesi UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Mripuko huo ulitokea katika eneo la Poltava katika bomba linalosafirisha gesi katika nchi nyingine za barani Ulaya na limetokea baada ya Urusi wiki hii kutangza kuwa imeikatia Ukraine gesi kutokana na deni na mzozo wa bei ya gesi hiyo.

Ukraine imesema inalichukulia shambulizi hilo kama kitendo cha kigaidi kinachonuia kutoa taswira kuwa nchi hiyo sio mshirika wa kuaminika wa kusambaza gesi.

Hata hivyo kampuni ya gesi ya Urusi Gazprom imesema usambazaji huo wa gesi kwa nchi za umoja wa Ulaya umeendelea leo bila ya matatizo yoyote kupitia bomba hilo la Poltav lililoshambuliwa.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Yusuf Saumu