Seif amtaka Magufuli aongoze rasmi mazungumzo Z′bar | Matukio ya Afrika | DW | 11.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Seif amtaka Magufuli aongoze rasmi mazungumzo Z'bar

Chama cha Wananchi (CUF) kimemuomba Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia moja kwa moja mazungumzo ya kusaka suluhisho la mkwamo wa kisheria na kikatiba visiwani Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Hoteli ya Serana, jijini Dar es Salaam, mapema leo (Januari 11), Katibu Mkuu wa CUF ambaye ndiye aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ametupilia mbali uwezekano wa kurejewa uchaguzi kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kuna kila dalili kuwa Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye anaongoza mazungumzo visiwani Zanzibar hataki kuitisha kikao cha mwisho kupokea tathmini ya vikao nane vilivyokwishafanyika tangu vilipoanza mwanzoni mwa mwezi Februari, na badala yake wasaidizi wake wanaandaa uchaguzi wa marudio kinyume cha sheria, jambo ambalo CUF haiko tayari.

Hakuna hoja ya kurudiwa uchaguzi

Rais John Magufuli wa Tanzania.

Rais John Magufuli wa Tanzania.

"Hoja ya kurudiwa kwa uchaguzi haina uhalali wa kisheria wala kikatiba. Ni jaribio la kuiingiza nchi kwenye machafuko. Ni kitendo cha kujaribu kumpa uhalali Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi kinyume cha sheria. Na hakikubaliki hata siku moja," alisema Maalim Seif kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na vyombo kadhaa vya habari ndani na nje ya Tanzania.

Kupitia mazungumzo hayo, Maalim Seif ambaye amegombea nafasi ya urais wa Zanzibar mara tano mfululizo kuanzia mwaka 1995, alisema uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 ulifanyika katika mazingira ya amani, haki na uhuru zaidi kuliko chaguzi nyengine huko nyuma, jambo ambalo lilisemwa pia na waangalizi wa ndani na wa kimataifa wa uchaguzi huo.

"Katika uchaguzi huo, ambao unakwenda sambamba na wa Muungano, mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM, John Magufuli alipata kura 194, 387 na (Edward) Lowassa (wa Chadema) alipata kura 211,033." Matokeo ya uchaguzi wa Muungano yaliendelea kama kawaida.

Ili kuukwamua mkwamo uliopo, Maalim Seif amemtaka Rais Magufuli kuingilia kati na kuongoza majadiliano hayo, kupitia vikao vya CCM na CUF, kwani mazungumzo ya sasa yameonesha udhaifu wa kimaamuzi.

Mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar ulianza mara tu baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kuufuta uchaguzi hapo tarehe 28 Oktoba 2015.

Mwandishi: Hawa Bihoga/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com