1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Redio za kijamii zasaidia kutoa elimu ya Ebola huko DRC

26 Mei 2026

Huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, upatikanaji wa mtandao wa intaneti katika maeneo ya vijijini bado ni changamoto kubwa.

https://p.dw.com/p/5EJjJ
Uhuru wa vyombo vya habari-mtangazaji wa Redio Okapi nchini Kongo
Mtangazaji katika Redio ya Kongo Okapi, inayoendeshwa na Umoja wa Mataif, .2015Picha: imago/photothek

Nje ya miji mikubwa kama Goma na Rutshuru, huduma ya intaneti ni karibu na sufuri. Wakaazi wa vijijini hawawezi kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp, na wala hawana televisheni. Redio za kijamii zinakuwa kiunganishi na dunia ya nje na baina ya jamii na jamii. Hali hiyo inatatiza upatikanaji wa taarifa sahihi, ambazo ni muhimu nyakati kama hizi za mripuko wa ugonjwa hatari wa Ebola.

Lakini zaidi ya habari, redio za kijamii pia zina jukumu muhimu katika kuhamasisha jamii na kuimarisha mshikamano wa kijamii, anaeleza Dieumerci Mumbere kutoka redio Updeco FM ya mjini Kiwanja.

"Tunafanya kazi moja kwa moja na wananchi. Kila siku, wakazi huja kueleza habari za maisha yao, kupitisha  matangazo na hata kusimulia juu ya matatizo yao. Redio, hapa kwetu, inakuwa kama sauti yao, na pia tunafanya mawasiliano na redio nyingine kama DW, RFI na hata Radio Okapi. Mnajua, katika kipindi hiki cha vita, sisi pia ni daraja kati ya mamlaka zilizopo na wananchi. Tumetekeleza jukumu kubwa katika kuleta hali ya utulivu. Wakati M23 ilipoanza kudhibiti eneo hili,  watu walikuwa na hofu kubwa kabisa.”

DR Kongo Bunia 2026 | Wafanyakazi wa shirika la Msalaba mwekundu wakiwa wamebeba jeneza la aliyekufa kwa Ebola Kongo
Wafanyakazi wa shirika la Msalaba mwekundu wakiwa wamebeba jeneza la aliyekufa kwa Ebola KongoPicha: Gradel Muyisa Mumbere/REUTERS

Redio za kijamii zinajaribu kustahimili shinikizo la kisiasa na kiusalama linalohusiana na kuingia kwa waasi hao wa AFC-M23 katika jimbo hilo. Lakini matatizo ya kiufundi na kifedha yanawasukuma baadhi ya wamiliki kupunguza wafanyakazi na kufuta baadhi ya vipindi. John Koraho ni mkurugenzi wa redio Alliance FM na anaeleza kwamba; 

"Tangu tulipoanza kuishi katika hali hii, tumepoteza washirika. Hali yetu ya kifedha ni mbaya sana. Hii inatuweka katika mazingira magumu kikazi. Wafanyakazi wanahitaji kupewa muongozo, lakini kwa kuwa hatuna tena rasilimali za kifedha wala washirika wa kutusaidia kuendesha redio, tulilazimika kupunguza wafanyakazi. Hii inatulazimu kutoa huduma ya kiwango cha chini kabisa.”

Kufungwa kwa redio katika maeneo yanayodhibitiwa na AFC-M23

Kwa mujibu wa takwimu za Mtandao wa Utetezi wa Vyombo vya Habari wa Kivu Kaskazini na Kivu Kusini (REPLAM), unaojumuisha zaidi ya vyombo 30 vya habari vya kijamii, zaidi ya redio 20 zimefungwa tangu mwaka 2022 katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa AFC-M23. Daniel Shematsi, mratibu wa mtandao huu, anatoa wito wa kuongeza msaada kwa redio za kijamii. Anasema hali inaashiria kuwa, katika miezi sita au mwaka mmoja, redio nyingine nyingi zinaweza kufungwa kutokana na hali ngumu ya maisha.

Shematsi anasisitiza kuwa katika mazingira ya migogoro, redio hizi za kijamii mara nyingi ndizo njia pekee ya kusambaza ujumbe wa amani, afya na maslahi ya umma, na kuuomba ulimwengu kusaidia kuvinusuru vyombo hivi muhimu vya habari.