1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa azikwa

Iddi Ssessanga
29 Julai 2020

Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa amezikwa kijijini Lupaso, wilaya ya Masasi mkoani Mtwara. Mkapa alifariki dunia wiki iliyopita kwa mstuko wa moyo akiwa hospitali alikokuwa anatibiwa ugonjwa wa Malaria.

https://p.dw.com/p/3g7SR
Tansania Trauerfeier des pensionierten Präsidenten William Mkapa
Picha: DW/S. Khamis

Mazishi ya rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa yamefanika katika kijiji alikozaliwa cha Lupaso, wilayani Masasi katika mkoa wa Mtwara kusini mwa Tanzania. Marehemu Mkapa alifariki usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 23 mwezi wa Julai jijini Dar es Salaam alikokuwa anatibiwa ugonjwa wa Malaria.

Mamia ya waombolezaji walijitokeza kuuaga mwili wa rais huyo kabla ya kusafirishwa kwenye kijijini Lupaso. Sherehe za kitaifa za kumuaga Mkapa zilifanyika jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwa ndege ya jeshi la anga la Tanzania hadi mkoani Mtwara.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na rais wa Tanzania John Magufuli pamoja na marais wastafu Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi, ambao wamemsifu kiongozi huyo kwa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa hilo, kupitia nafasi mbalimbali alizozishikilia.

Tansania Trauerfeier des pensionierten Präsidenten William Mkapa
Rais Magufuli na rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi wakitoa heshima zao kwa jeneza na Hayati Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Julai 28, 2020.Picha: DW/S. Khamis

Magufuli awataka Watannzania kumuombea Mkapa

Rais wa Tanzania John Magufuli amewataka watanzania waendelee kumuombea Rais Mkapa na kuwasisitiza kuiga tabia zote njema alizokuwa nazo wakati wa uhai wake ikiwa pamoja kuwa mzalendo wa kweli na kupenda nyumbani kwao.

Magufuli amesema Mkapa aliyaishi maisha yenye upendo wa kweli na alipenda nyumbani kwao kwani hata pale serikali ilivyojaribu kutenga eneo maalumu la kuzikia viongozi wa kitaifa jijini Dodoma alipinga wazo hilo na kuagiza atakapofariki azikwe kijijini kwao kwenye makaburi ya familia.

Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete amemuelezea Hayati Benjamin Mkapa kama kiongozi aliyechukia nchi na watu wake kuwa maskini na kulipa kipaumbele suala la uchumi na kupelekea kuanzisha dira ya taifa ya kufikia uchumi wa kati ifakapo mwaka 2025 na pato la mtanzania kufikia dola 3000.

Ameongeza kuwa  Hayati Benjamin Mkapa alikuwa kiongozi mwenye utambuzi na manufaa kwa wananchi wake kwa kuwa alipenda kusikiliza, kushughulikia changamoto na kutoa mrejesho.

Tansania Trauerfeier des pensionierten Präsidenten William Mkapa
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akishiriki shughuli ya kuuaga mwili wa rais mstaafu Benjamin Mkapa, katika uwanja wa taifa, ambao hivi ni uwanja wa Mkapa.Picha: DW/S. Khamis

Soma pia Wajue Marais wa Zamani wa Tanzania

Mwinyi: Mkapa alikuwa binadamu

Akizungumza katika shughuli ya mazishi ya Mkapa, rais mstaafu wa awamu ya pili. Mzee Ali Hassan Mwinyi alisema hayati Benjamin Mkapa alikuwa mwanadamu na ana makosa yake kama wengine hivyo aombewe kwa Mwenyezi Mungu.

"Huenda alifanya makosa asiyopenda Muumba wetu, tumuombee msamaha kwa mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake, amuwie radhi, Mkapa alikuwa mtu mwema na mkrimu, asiependa masihara kwenye kazi," alisema Mwinyi.

Wazanzibari watangaza kumsamehe

Baadhi ya waathirika wa maandamano ya kisiasa ya kudai haki ya kidemokrasia yaliyotokea mwaka 2001 Unguja na Pemba ambao wanaendelea kubaki na makovu ya risasi mwilini wametangaza kumsamehe Rais Mkapa.

Tansania - Burundi Friedensgespräche mit Benjamin Mkapa
Hayati Mkapa enzi za uhai wake akiwa msuluhishi wa mzozo wa Burundi.Picha: Charles Ngereza

Soma pia Hisia kutoka Zanzibar kuhusu kifo cha Benjamin Mkapa

Wanasiasa waliokuwa wafuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF) akiwemo Kiongozi wa vijana Said Miraji na Fathia Zahrani wametangaza kumsamehe kiongozi huyo ambaye ndiye aliyekuwa Amiri Jeshi mkuu, katika ghasia hizo zilizotokea Januari 26/27 2001 ambapo watu kadhaa walipoteza maisha na wengi kukimbilia Mombasa Kenya.

Licha ya kusamehe waathirika hao wameziomba serikali kutekeleza mapendekezo ya Tume kwenye kipengele cha kuwalipa fidia ambacho ni muhimu katika kupunguza maumivu. Tume ya uchunguzi wa mauaji hayo ilisema watu 30 waliuawa.
 

Mkapa alikuwa rais wa Tanzania wa awamu ya tatu kwa miaka kumi kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, na limuachia rais Jakaya Kikwete kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 2015, alipochaguliwa rais wa sasa John Magufuli.

Mkapa amezikwa kwa taratibu za kijeshi ambapo amepigiwa mizinga 21.

Salma Mkaliba kutoka Mtwara na Salma Said kutoka Zanzibar wamechangia kwenye ripoti hii.