Rais wa Marekani Barrack Obama akutana na Papa Francis | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Marekani Barrack Obama akutana na Papa Francis

Rais wa Marekani Barrack Obama leo yuko nchini Italia katika ziara ya siku sita barani Ulaya. Obama amekutana kwa mara ya kwanza na kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis katika makao makuu ya kanisa hilo ya Vatikani

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo kuhusu ajenda kadhaa ikiwemo kutokuwepo kwa usawa katika jamii.

Mazungumzo hayo ya kwanza kati ya Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na Rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika yataangazia pengo kubwa lililko kati ya maskini na matajiri duniani na pia wanatarajiwa kugusia masuala nyeti kama uavyaji mimba,ushoga , matumizi ya mbinu za kupanga uzazi,mchakato wa amani Mashariki ya Kati na uhamiaji.

Obama amesema amefurahishwa kukutana na Papa ambaye amemtaja kielelezo chema kwa watu wengi ulimwenguni akiwemo yeye.Obama anaandamana na waziri wake wa mambo ya nje John Kerry katika ziara hiyo ya Vatican miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi ya juu wa serikali yake.Obama ndiye rais wa tisa wa Marekani kufanya ziara rasmi katika makao makuu ya kanisa Katoliki.

Obama kukutana pia na viongozi wa serikali ya Italia

Obama pia atakutana na waziri mkuu mpya wa Italia Matteo Renzi na Rais wa Italia Giorgio Napolitano.Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Italia ni mzuri licha ya Italia kuhitaji kushawishika zaidi kuhusu athari za kuiwekea Urusi vikwazo kwa uchumi wake.

Rais wa Marekani Barrack Obama akiwa Brussels

Rais wa Marekani Barrack Obama akiwa Brussels

Hapo jana akiwa mjini Brussels,Rais huyo wa Marekani alizihimiza nchi za magharibi kusimama kidete katika kuipinga hatua ya Urusi kulidhibiti eneo la Crimea akisema baada ya muda Urusi itatambua kuwa matumizi ya nguvu hayawezi kushinda.

Akiuhutubia umati wa kiasi ya watu 2,000 mjini Brussels,nchini Ubelgiji, Obama alisema hatua ya Urusi imekiuka imani kuwa haki za kimataifa zinazingatiwa,mipaka haiwezi kubatilishwa na kwamba watu wanaweza kuamua hatma ya maisha yao ya baadaye.

Nchi za magharibi ziungane

Mapema mjini Brussels,Obama alifanya mkutano wa dakika tisini na maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya ambapo alitoa wito kwa Ulaya na Marekani kuungana kama kitu kimoja.

Ziara hii ya Obama barani Ulaya inaonekana kuwa muhimu sana kutokana na mzozo unaoendelea kuihusu Ukraine na mkutano huo na viongozi wa Umoja wa Ulaya ulikuwa mkutano wa kwanza wa kilele uliofanywa na Obama pamoja na Rais wa tume ya Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy na Jose Manuel Barosso.

Rais Obama na viongozi wa Umoja wa Ulaya

Rais Obama na viongozi wa Umoja wa Ulaya

Kiongozi huyo wa Marekani alisema mzozo wa Ukraine umefichua suala la kuwa nchi kadhaa za umoja wa Ulaya zinaitegemea pakubwa Urusi kwa ajili ya nishati na kusema kuna haja ya kutafuta njia mbadala kukidhia mahitaji hayo ya gesi na nishati.

Suala jingine ambalo lilijadiliwa katika mkutano huo wa Brussels ni madai ya kuwa shirika la kitaifa la usalama la Marekani lilidukua mawasiliano ya raia wa Ulaya.

Italia ndiyo kituo cha mwisho cha ziara ya wiki nzima ya Rais huyo wa Marekani,ziara ambayo ilianzia Uholanzi na kisha kuelekea Ubelgiji.Obama anatarajiwa kuondoka Italia hapo kesho kuelekea Saudi Arabia.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com