Rais Mugabe hataki kung′atuka | Magazetini | DW | 25.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Rais Mugabe hataki kung'atuka

Mugabe na kiu cha kuendelea na madaraka, uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini Mali na mkataba wa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika ni miongoni mwa mada za Afrika katika Magazeti ya Ujerumani wiki hii

Tunaanzia Zimbabwe ambako rais Robert Gabriel Mugabe mwenye umri wa miaka 92 anakishinikiza chama chake kikubali agombee tena wadhifa wake uchaguzi utakapoitishwa mwaka 2018."Mugabe anataka kwenda tena" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Berlin die tageszeitung linaloandika " muda mfupi kabla ya uchaguzi mdogo unaopewa umuhimu mkubwa nchini Zimbabwe,na kabla ya kuitishwa mkutano mkuu wa chama tawala cha Zanu/PF,mjadala umezidi makali kuhusu mustakbal wa rais aliyezeeka Robert Mugabe anaeiongoza Zimbabwe tangu uhuru mwaka 1980. Kundi la wakosoaji wanakitolea wito chama chao kimteuwe kiongozi mbadala atakaekiongoza chama cha Zanu/PF uchaguzi utakapaoitishwa mwaka 2018. Lakini hadi wakati huu,linaendelea kuandika gazeti la die tageszeitung rais Mugabe amekuwa akifanikiwa kuwafumba midomo wapinzani wake chamani.

Mugabe anataka kuwazuwia waingereza na wamerekani wasirejeshe ukoloni Zimbabwe

Mugabe anataka kwa kila hali kugombea mhula ziada,licha ya kwamba uchaguzi utakapoitishwa atakuwa na umri wa miaka 94 linaendelea kuandika gazeti hilo la mjini Berlin na kumnukuu rais Mugabe akisema mwishoni mwa wiki iliyopita "hatong'atuka". Sababu anazotoa ni pamoja na kile anachokiitaja kuwa " kuwazuwia wakoloni wa zamani Uingereza na Marekani kuitawala upya ZImbabwe."Tuko katika wakati mgumu ambapo wamarekani na waingereza wanachochea mageuzi ya serikali" amesema Mugabe  kwa lugha ya kienyeji ya shona mbele ya "mashujaa wa vita vya ukombozi vya miaka ya 70."Nikibidi kustaafu,kwa hisani zenu niacheni nistaafu ipasavyo,bila ya kuwepo mabadiliko ya serikali....ikiwa nimeiteketeza nchi,nambieni ili nipate kwenda zangu-nnajua baadhi yenu wanajiandaa kurithi wadhifa wangu na wangependa kuona nnafariki,lakini nifariki kwanini?",amejiuliza. Hata hivyo wawakilishi wa mashujaa wa vita vya ukombozi, linaandika die Tagesazeitung hawatounga mkono fikra ya Mugabe kugombea mhula mwengine,wanatoa sababu za uzembe na rushwa.

Uamuzi kuhusu mustakbal wa Mugabe utapitishwa mkutano mkuu wa chama tawala cha Zanu /PF utakapoitishwa mwezi unaokuja, mkutano utagharimu dala milioni nne za kimarekani ambazo wananchi licha ya hali yao duni wanabidi waugharimie.Die Tageszeitung limeyanukuu mashirika ya haki za binaadam yakisema kila raia mmoja wa vijijini anatakiwa achangie senti 50 katika fuko la chama la sivyo atafutwa katika orodha ya wanaopatiwa misaada ya chakula.

Machafuko yameripuka upya Mali

Uchaguzi pia nchini Mali ambako die Tageszeitung linasema umezusha kishindo kikubwa. Uchaguzi huo wa mabaraza la miji umewapatia nafasi waasi kubainisha baado wapo. Die Tageszeitung linasema uchaguzi huo umetumiwa na serikali pia kudhihirisha nguvu zake katika ardhi yote ya Mali. Uchaguzi uliyahusu maeneo 688 kati ya 708 . Wapiga kura milioni 7 na laki mbili walitakiwa wayachague mabaraza 12.000 ya miji. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa uchaguzi kama huo wa mabaraza ya miji kuitishwa tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2012 na 2013. Mitihani imetokea pale makundi ya wanamgambo wa itikadi kali katika maeneo ya kaskani mwa Mali walipotoa wito wa kususiwa uchaguzi huo. Serikali ya rais Ibrahim Boubacar Keita ilipinga ikihoji uchaguzi huo umeshaakhirishwa mara nne. Hatimae hakuna aliyefaidika na uchaguzi huo,ambao hadi leo matokeo yake hayakutangazwa. Wanajeshi watano na raia mmoja wameuwawa linamaliza kuandika die Tageszeietung.

Makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika

Ripoti yetu ya mwisho inahusu ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya Afrika. Gazeti la Süddeutsche limezungumzia makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa na kumnukuu kamishna wa Umoja wa ulaya Cecilia Malmström akilisifu bara la Afrika kuwa bara la matumaini. Makubaliano kama haya yanakusudiwa pia kuimarisha matumaini hayo amenukuliwa Cecilia Malmström akisema.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri:Yusuf Saumu