1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Erdogan alaani mashambulizi ya bomu katika jiji la Ankara

Zainab Aziz
1 Oktoba 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelielezea shambulio la bomu la kujitoa mhanga la jijini Ankara kama pumzi ya mwisho ya magaidi.

https://p.dw.com/p/4X1Oa
Türkei Erdogan Rede Parlament
Picha: AFP

Erdogan ameyasema hayo kwenye hotuba yake kwa wabunge waliokutanika tena bungeni baada ya mapumziko ya majira ya joto.

Kwa mujibu wa shirika la Habari la serikali ya Uturuki Anadolu, Erdogan amesema wahusika hawakufikia malengo yao na kamwe hawatafanikiwa.

Bunge la Uturuki katika mji mkuu, Ankara
Bunge la Uturuki katika mji mkuu, AnkaraPicha: Evrim Aydin/AA/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amesema mashambulio ya siku ya Jumapili yamewahusisha watu wawili.

Mshambuliaji wa kwanza alikufa baada ya kujitoa mhanga alitumia kifaa cha kulipuka katika eneo la katikati mwa mji mkuu wa Uturuki, Ankara, siku ya Jumapili.

Mwenzake aliuawa katika majibizano ya risasi kati yake na polisi.

Soma pia:Mshambuliaji ajitoa mhanga katikati mwa mji mkuu wa Uturuki

Jumuiya ya kujihami ya NATO ambayo Uturuki ni mwanachama imesisitiza kuwa inasimama pamoja na Uturuki katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amelaani shambulizi  la Jumapili dhidi ya Wizara ya Mambo ya Ndani huko Ankara na amewatakia ahueni ya haraka maafisa wa polisi waliojeruhiwa.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Uturuki imefanya operesheni kadhaa kaskazini mwa Syria tangu mwaka 2016 kuwafukuza wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS na wanamgambo wa Kikurdi, YPG, kutoka kwenye mpakani.

Uturuki inalichukulia kundi hilo la YPG kama washirika wa chama cha PKKkilichopigwa marufuku. Chama hicho cha PKK  kimeorodheshwa kwenye makundi ya kigaidi na Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya. Wapiganaji wa PKK wanaendesha uasi dhidi ya Uturuki tangu mwaka 1984.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amesema serikali ya Uturuki itaendelea na mapambano dhidi ya magaidi, washirika wao, walanguzi wa madawa ya kulevya, na magenge ya uhalifu.

Rais wa Uturuki  Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Mustafa Kamaci/AA/picture alliance

Hata hivyo waziri huyo wa Mambo ya Ndani hajasema mpaka sasa aliyehusikja na mashambulio ya Jumapili karibu na wizara yake na Bunge katika mji mkuu Ankara.

Vyanzo:DPA/AP/AFP