1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaSyria

Rais Erdogan akiri shughuli za uokozi zinakwenda taratibu

Sylvia Mwehozi
10 Februari 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelitembelea jimbo la Adiyaman kukagua shughuli za uokozi na utoaji wa misaada zinazoendelea. Ametangaza msamaha wa kodi za nyumba kwa wahanga wa tetemeko kwa kipindi cha mwaka mmoja

https://p.dw.com/p/4NL04
Türkei  | Präsident Recep Tayyip Erdogan in Kahramanmaras
Picha: Mustafa Kamaci/AA/picture alliance

Akizungumza mjini humo Erdogan amekiri kwamba shughuli za uokozi zinazofanywa na serikali yake zinakwenda taratibu kinyume na ilivyotarajiwa. Ametangaza msamaha wa kodi za nyumba kwa wahanga wa tetemeko kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwamba majengo mapya yatajengwa ndani ya mwaka mmoja.

"Kwa bahati mbaya kulingana na takwimu za hivi karibuni, idadi ya raia wetu waliofariki katika majimbo 10 imepanda na kufikia elfu 18.991 na idadi ya manusura ni elfu 75,523. Tumedhamiria kujenga upya majengo yote yaliyobomoka ndani ya mwaka mmoja. tutahakikisha wananchi wetu wanaoishi katika mahema wanahamia katika majengo na tutalipa kodi." alisema Erdogan.Idadi ya watu waliofariki hadi sasa imetajwa kufikia karibu 22,000.

Türkeiund Syrien | Unterkunft für Überlebende des Erdbebens in Kharamanmaras
Raia wakiwasili katika Mahema ya muda mjini Kharamanmaras kusini mashariki mwa Uturuki Picha: Kamran Jebreili/AP Photo/picture alliance

Wakati huo duru zinasema Uturuki inajadili juu ya kuufungua tena mpaka unaovuka kuingia katika eneo linalodhibitiwa na serikali ya Syria ili kuwezesha usambazaji wa misaada wakati rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akikiri kwamba shughuli ya uokozi inajikongoza kinyume na ilivyotarajiwa. Wakati huo huo kuna shutuma kwamba Syria imetengwa katika upewaji wa misaada ya kibinadamu katika mkasa huu wa tetemeko la ardhi.Watu sita wakutwa hai baada ya kunasa katika kifusi Uturuki

Afisa mmoja wa Uturuki ambaye hakutaka jina lake kutajwa amesema kuwa mpaka unaovuka kutoka jimbo la Hatay kuelekea eneo linaloshikiliwa na serikali ya Syria katika jimbo la Latakia unaweza kufunguliwa tena. Uturuki inapanga pia kuifungua tena njia nyingine inayoshikiliwa na upinzani kwenye mkoa wa Idlib. Kwa hivi sasa kuna njia moja tu ya mpaka wa Bab al-Hawa iliyofunguliwa kati ya Uturuki na maeneo ya wapinzani kaskazini magharibi mwa Syria. Umoja wa Mataifa umeeleza kwamba usambazaji wa misaada kupitia mpaka huo ni "mkombozi" kwa watu milioni 4 ambao unasema tayari walikuwa wakitegemea msaada wa kibinadamu kabla ya tetemeko la ardhi na kwamba mahitaji hayo sasa yameongezaka.

Vifaa duni vyakwamisha uokozi Syria

Hata hivyo mkuu wa shirika la kofia nyeupe la nchini Syria Raed Al Saleh ameushutumu Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kupeleka misaada ya kiutu inayohitajika katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi huko Syria. Amesema msafara wa malori ulioingia jana ulikuwa umepangwa kuwasili siku ya Jumatatu lakini ulichelewa kutokana na tetemeko la ardhi. Saleh ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuwaomba radhi watu wa Syria kwa ukosefu wa msaada.Majengo ya zamani, matetemeko madogo yalisababisha zahma Uturuki na Syria

Nayo wizara ya fedha ya Marekani imetoa idhini ya kuruhusu misaada ya tetemeko la ardhi kwa ajili ya Syria ambayo ingezuiliwa kutokana na vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Naibu waziri wa fedha wa Marekani Wally Adeyemo amesema kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Syria haviwezi kuzuia juhudi za kuokoa maisha huko Syria, wakati washirika wa kimataifa na mashirika ya kiutu wakihimiza kuwasaidia walioathirika.

Soma: Tetemeko la ardhi: Juhudi za uokoaji zaingia siku ya nne

Syria imegubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 12 sasa huku vikwazo vilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya vikitatiza mauzo nchini humo. Tangu Jumatatu maafisa wa serikali ya Syria wametoa rai kwa jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo hivyo ambavyo inavitaja kuwa vinasababisha ukosefu wa rasilimali na vifaa vizito vya kuondoa vifusi wakati wa zoezi la uokoaji.