1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais amteua waziri mkuu anaendoka Poland kuunda serikali

Iddi Ssessanga
7 Novemba 2023

Rais wa Poland amempa waziri mkuu wa sasa jukumu la jaribio la kwanza la kuunda serikali mpya baada ya chama tawala cha kihafidhina, PiS, kushinda uchaguzi mwezi uliopita, lakini hakikupata wingi wa kutosha wa wabunge.

https://p.dw.com/p/4YVZs
Uundwaji wa serikali Poland
Rais wa Poland Andrzej Duda.Picha: Beata Zawrzel/NurPhoto/picture alliance

Chama cha Sheria na Haki, PiS, kiliibuka cha kwanza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 15, lakini bila wingi wa wazi na kikiwa nafasi ndogo ya kuunda muungano.

"Nimeamua kukabidhi jukumu la kuunda serikali kwa Waziri Mkuu Mateusz Morawiecki," alisema Rais Andrzej Duda, ambaye anashirikiana na wahafidhina walio madarakani.

"Endapo misheni ya mwakilishi wa chama cha Sheria na Haki haitafanikiwa, basi katika awamu inayofuata bunge litamchagua mgombea wa uwaziri mkuu na nitamteua bila kuchelewa," aliongeza, katika hotuba yake ya televisheni.

Soma pia: Rais wa Poland kumtangaza waziri mkuu mpya

Morawiecki alimshukuru rais kwa kumwamini katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Facebook.

Kambi ya kiongozi wa upinzani Donald Tusk ya kiliberali ya Muungano wa Kiraia, KO, ilimaliza katika nafasi ya pili lakini pamoja na vyama viwili vidogo -- chenye msimamo wa wastani, Third Way na cha mrengo wa Kushoto -- vilipata wingi wa wabunge 248 katika bunge hilo lenye viti 460.

Warsaw| Mwansiasa Donald Tusk
Kiongozi wa muungano wa Kiraia, KO, Donald Tusk, amemshtumu Rais Duda kwa kuchelewesha uundwaji wa serikali kwa hatua yake ya kumpa jukumu waziri mkuu wa sasa kujaribu kuunda serikali.Picha: Attila Husejnow/SOPA/IMAGO

Tusk, ambaye ni waziri mkuu wa zamani na mkuu wa zamani wa Baraza la Ulaya, amemshutumu Duda kwa "kuchezea wakati".

Soma pia: Muungano wa upinzani wafanikiwa wingi wa viti Poland

Viongozi wa muungano wa upinzani wa kiliberali kwa pamoja walikuwa wametoa wito kwa Duda kumteua Tusk.

Haijulikani ni chama gani PiS, ambayo ilipata viti 194, inaweza kutawala nacho wakati waangalizi wanaona kukosekana kwa washirika wanaofaa wa muungano.

Alirudia shtuma hizo Jumatatu kwenye mkutano wa hadhara kabla tu ya tangazo la Duda, mara tu vyombo vya habari vya ndani vilipofichua uamuzi wa mkuu huyo wa nchi.

"Rais alisema atamteua Morawiecki... Kwa hivyo kama nilivyosema, watataka kuiba siku chache," Tusk aliwaambia wafuasi wake katika mji wa kusini magharibi wa Wroclaw.

Tusk alidai kuwa hatua hiyo "haitabadilisha chochote", akipendekeza kwamba yeye mwenyewe hatimaye atakuwa mkuu wa serikali.

Hata hivyo, alisema madai ya kukwama ni aibu kwa sababu kwa sasa wakati ni jambo la msingi kwa Poland: "Kila siku inayopotea ni hasara kwa nchi yetu, hasara kwa Wapoland wote."

Poland| Andrzej Duda na Mateusz Morawiecki
Rais wa Poland Andrzej Duda, kushoto, akikutana na Waziri Mkuu Mateusz Morawiecki, kutoka chama tawala cha Haki na Sheria, PiS, kuzungumzia uundwaji wa serikali mpya, Oktoba 24, 2023.Picha: JANEK SKARZYNSKI/AFP

Soma pia: Tusk aibuka mshindi uchaguzi Poland

Wakati wa kampeni za uchaguzi, Tusk alikuwa ameahidi kujenga upya uhusiano na Umoja wa Ulaya na kufungulia fedha za Umoja wa Ulaya zilizokuwa zimefungiwa ifikapo Desemba. Mwezi uliopita, Tusk alikutana na mkuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen mjini Brussels kujadili suala hilo.

Alisisitiza kwamba washirika wake wameonyesha "kwamba kupinga demokrasia na kupinga Ulaya hakupaswi kuwa mtindo, kwamba ni misukosuko tu ya msimu".

Uhusiano wa Poland na taasisi zinazosimamia Umoja wa Ulaya umeporomoka tangu PiS ilipoingia madarakani kutokana na hisia kuwa Warsaw ilikuwa inarudisha nyuma demokrasia.

Brussels ilikuwa imeizuilia Poland kiasi cha euro bilioni 35 katika fedha za ufufuaji wa kiuchumi kufuatia janga la UVIKO-19 katika Umoja wa Ulaya, kwa sababu ya mzozo juu ya mageuzi ya mahakama.

Chanzo: Mashirika