Putin akutana na Poroshenko | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Putin akutana na Poroshenko

Rais Vladimir Putin wa Urusi amekutana na mwenzake wa Ukraine, Petro Poroshenko, kujadiliana mzozo kati ya nchi zao, lakini Kremlin ikisema ni mazungumzo yaliyojaa utata na suintafahamu.

Rais Vladimir Putin wa Urusi (kushoto) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakiingia kwenye ukumbi wa mkutano kati ya Urusi, Ukraine na Umoja wa Ulaya.

Rais Vladimir Putin wa Urusi (kushoto) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakiingia kwenye ukumbi wa mkutano kati ya Urusi, Ukraine na Umoja wa Ulaya.

Viongozi hao wawili walikutana mapema Ijumaa (17 Oktoba) kandoni mwa mkutano wa kilele kati ya Ulaya na Asia kabla ya kufanya majadiliano makubwa zaidi na viongozi wa Umoja wa Ulaya ambao wametiwa shaka sana na ambavyo mzozo baina yao unavyoweza kuzua mtafaruku kwenye kiwango cha kimataifa.

Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, ambaye ndiye aliyeitisha mazungumzo hayo ya leo, yaliyofanyika kwenye ukumbi ulio mbali na ule unakofanyika mkutano wa kilele, amesema mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron. Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, pia walihudhuria.

Muda mchache kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa mkutano, Rais Poroshenko alisema mazungumzo hayo yalihusiana na ajenda zote muhimu ambazo zimezua mzozo kati ya nchi yake na Urusi kwa siku za hivi karibuni. "Masuala muhimu yakiwemo yale ya amani, kutekelezwa kwa ukamilifu makubaliano ya Misk, usitishaji mapigano, kuondoa wanajeshi na kuheshimiwa kwa mamlaka ya Ukraine, na kando ya hayo ni kutatuliwa kwa masuala ya nishati."

Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi (katikati) akimkaribisha Rais Petro Poroshenko wa Ukraine.

Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi (katikati) akimkaribisha Rais Petro Poroshenko wa Ukraine.

Renzi aliyaelezea mazungumzo hayo kuwa ya kutia moyo na kwamba ana matumaini ya kuukwamua mkwamo uliopo.

"Tulitaka kufikia mahala pa kuona kuwa kuna mabadiliko kwenye namna tunavyouzungumzia mzozo nchini Ukraine. Nadhani tumepiga hatua moja mbele kutokana na mazingira yaliyopo kwa maslahi ya majadiliano yanayojenga. Hapana shaka kwamba kuna tafauti nyingi. Hilo ni jambo la kawaida," alisema Renzi.

Urusi yasema mazungumzo magumu

Lakini msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov, aliyaelezea mazungumzo hayo kuwa ni magumu sana. Akizungumza na waandishi wa habari, Peskov alisema: "Mazungumzo haya kwa hakika ni magumu. Kuna suintafahamu nyingi na kiwango kikubwa cha kutokukubaliana. Hata hivyo yanaendelea."

Mataifa ya Magharibi yaliiwekea vikwazo Urusi kwa kuichukuwa kwake Rasi ya Crimea mapema mwaka huu na kwa kile wanachosema ni kuunga mkono kwake waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine. Mzozo huu unatajwa na wachambuzi kwamba unakaribiana sana na siasa za Vita Baridi.

Ulaya inahofia kwamba uamuzi wa Urusi kuikatia gesi Ukraine kwa sababu ya kutokulipia, kunaweza kuathiri mgao wa gesi kote barani Ulaya kwenye majira ya baridi yanayokaribia na sasa unapigania kufikiwa kwa makubaliano.

Urusi ndiye msambazaji mkubwa wa gesi kwa Ulaya, ikiwa inatoa kiasi cha robo nzima ya gesi inayotumika, huku nusu yake ikiwa inapitia Ukraine.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com