Pence asema wahafidhina wana fursa ya kihistoria | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Pence asema wahafidhina wana fursa ya kihistoria

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amesema Marekani imepata fursa ya kipekee kutatua matatizo yanayoikabili nchi hiyo kwa kutumia majibu ya chama cha Republican baada ya chama hicho kudhibiti urais na bunge.

Pence aliyasema hayo katika mkutano wa vuguvugu la wahafidhina unaofanyika mjini Oxon Hill ambao unatarajiwa kuhutubiwa na rais Donald Trump hii leo. Pence aliutaja ushindi wa Trump katika uchaguzi wa mwaka jana kuwa ni fursa ya maisha na hivyo kuwataka wanaharakati wa kihafidhina kutoiharibu fursa hiyo.

Makamu wa rais Pence alisema utawala mpya wa Trump umewapa fursa wahafidhina kuonyesha kwamba majibu yao ndiyo sahihi kwa Marekani. Pence alisema utawala huo mpya utaiondoa sheria ya huduma za afya na kuanzisha nyingine mbadala, akisema jinamizi la taifa la Obamacare linakaribia kufika mwisho. Lakini aliongeza kuwa wahafidhina wanapaswa kujiandaa na mapambano dhidi ya Wademocrat.

USA National Harbor, Maryland Steve Bannon bei CPAC (Getty Images/A. Wong)

Mkuu wa shughuli za ikulu ya White House Reince Priebus akizungumza wakati wa mkutano wa CPAC, Maryland.

"Ndani ya timu hii, sisi wahafidhina tunayo fursa ambayo inakuja kila baada ya vizazi vichache, au inaweza kuja mara moja tu katika maisha. Marafiki zangu, hii ndiyo  fursa tuliyoisubiri kwa muda mrefu. Huu ndiyo wakati wa kuonyesha kwa mara nyingine kwamba majibu yetu ndiyo majibu sahihi kwa Marekani. Jeshi imara, nafasi zaidi za ajira, kodi kidogo, kuheshimu katiba na maadili yalioifanya Marekani kuwa taifa kubwa na imani kubwa katika uzuri wa watu wa Marekani," alisema Pence.

Mashaka ya wahafidhina kwa Trump

Mapema mkuu wa shughuli za ikulu Reince Priebus aliomba uvumilivu na umoja, akiwasihi wanaharakati kutofuja udhibiti wa Warepublican wa mabaraza yote ya bunge pamoja na ikulu ya White House. Mshauri wa Trump Steve Bannon aliwasilisha hoja ya kuwa mkakati wa utawala wenye msingi wake katika kupunguza utitiri wa sheria na uzalendo wa kiuchumi katika kujadili mikataba mipya ya kibiashara.

Utetezi wa Priebus umetambua mashaka ya wahafidhina kuhusu rais huyo mpya, mwanachama wa zamani wa chama cha Democratic ambaye huko nyuma alikuwa akizomewa aktika mkutano huo. Trump ameonyesha mara kwa mara kuwa hatoi kipaumbele kwa masuala ya kijamii ambayo wahafidhina wengi wanayapa umuhimu, na pendekezo lake la uwekezaji mkubwa katika miundombinu limetia mashaka dhamira yake ya kupunguza matumizi ya serikali.

USA CPAC-Treffen - Konferenz der Konservativen (DW/M. Shwayder)

Wajumbe wakielekea kwenye mkutano wa CPAC

Lakini wakati ambapo Mrepublican akikalia kiti cha rais kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka nane, wanaharakti wengi wanasema wanahisi wana nguvu na wako tayari kumpa nafasi. Vuguvugu la wanaharakati wa kihafidhina lililoanzishwa muongo mmoja uliopita limekuwa kama kamati ya ushawishi.

Rais Trump anatarajiwa kuhutubia mkutano huo ulioingia katika siku ya tatu leo, akilenga kuimarisha ushawishi wake katika jukwaa ambalo kw amuda mrefu limetafuta njia za kubadilisha mfumo wa sheria za kodi za Marekani, kupunguza utitiri wa sheria za udhibiti wa biashara na kufuta sheria ya huduma za afya ya rais wa zamani wa Demcratic Barack Obama.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,ape

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com