1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pelosi atoa idhini kutayarishwa mashtaka dhidi ya Trump

Admin.WagnerD6 Desemba 2019

Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi ametoa ruhusa ya kutayarishwa kwa ibara za mashtaka dhidi ya rais Donald Trump, hatua muhimu katika mchakato wa kujaribu kumuondoa madarakani rais huyo wa chama cha Republican. 

https://p.dw.com/p/3UJTq
USA Nancy Pelosi
Spika wa Bunge la Marekani, Nancy PelosiPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Scott Applewhite

Katika mkutano wake na waandishi habari mjini Washington jana Spika Pelosi amesema atawaomba viongozi wa Bunge kuendelea na mipango ya kutayarisha orodha ya mashtaka dhidi ya Trump ambayo itajumuisha ushahidi uliopatikana kuhusiana na jinsi rais huyo alivyojishughulisha na suala la Ukraine.

Pelosi amesema matendo ya Trump katika suala la msaada wa ulinzi kwa Ukraine yamekiuka kwa sehemu kubwa misingi ya taifa na kiapo cha ofisi.

"Taarifa zilizozopo hazina ubishi, ukweli ni kwamba rais alitumia madaraka yake vibaya kwa maslahi binafsi na manufaa ya kisiasa kwa kuweka rehani usalama wetu wa taifa alipozuia msaada wa kijeshi na kutoa nafasi ya mkutano muhimu kwenye ofisi ya rais ili litolewe tangazo la kumchunguza hasimu wake wa kisasia." alisema Pelosi.

Uamuzi wa Pelosi umekuja siku moja baada ya wanazuoni watatu wa masuala ya katiba kuwaarifu wabunge kwamba wanaamini rais Trump amefanya makosa ya kiwango cha kuweza kushtakiwa na kuondolewa chini ya katiba ya nchi hiyo.

Pelosi: Trump amepoteza imani ya umma

Bildkombo Nancy Pelosi und Donald Trump Impeachment

Pelosi amesema ushahidi uliotolewa hauna shaka kwamba matendo ya kiongozi huyo ni ukiukwaji mkubwa wa imani ya umma na uvunjaji wa kiwango cha juu wa misingi ya katiba.

Trump anatuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kuendesha kampeni iliyowahusisha washirika wake wa ndani ya kuishinikiza Ukraine ipekue uozo dhidi ya mpinzani wake wa kisiasa kutoka chama cha Demcratic, Joe Biden.

Trump anashutumiwa kumtaka rais mpya wa Ukraine Volodymyr Zelensky atangaze kuanzisha uchunguzi dhidi ya mtoto wa Biden, aliyefanya kazi na kampuni ya nishati nchini Ukraine kama sharti la kupatiwa msaada wa ulinzi na kukaribishwa kwa ziara rasmi mjini Washington.

Mashtaka dhidi yake yanaweza kujumuisha matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kuzuia utoaji wa haki.

Trump awashambulia wademocrats 

Donald Trump
Picha: picture-alliance/ZumaPress/SOPA Images/P. Hennessy

Rais Trump mwenyewe amejibu uamuzi huo wa bunge  kwa kusema kupitia ukurasa wa Twitter kuwa wademocrats wanataka kumuondoa madarakani bila kuweko sababu ya msingi na  kwamba  matumaini ya kushinda kwa sababu chama chake cha Republican kimeungana vya kutisha dhidi ya mchakato huo.

Baraza la Seneti linalodhibitiwa na Republican ndiyo litakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusiana na mashtaka ya rais na sharti ni kwamba theluthi mbili ya kura za maseneta inahitajika kuweza kumuondoa rais Trump madarakani.

Warepublicans wamekwisha sema hakuna ushahidi wa kutosha kwamba Trump alifanya makosa yanaweza kumtoa madarakani na kwamba wademocrats wanaoendesha mchakato huo wameruhusu hisia na chuki dhidi ya kiongozi huyo kutawala maaumuzi wanayofikia.