Papa: Wakristo na Waislamu ni ndugu | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papa: Wakristo na Waislamu ni ndugu

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis amesema Wakristo na Waislamu ni ndugu, hivyo amewataka wakatae chuki na kuungana pamoja kupinga ghasia zinazofanywa kwa kisingizio cha kutumia jina la dini.

Papa Francis akiwa katika msikiti wa Bangui

Papa Francis akiwa katika msikiti wa Bangui

Akizungumza leo wakati akiuzuru msikiti wa Koudoukou uliopo kwenye wilaya ya PK5 katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, Papa Francis amesema Wakristo na Waislamu ni kaka na dada na kwamba wale wanaodai kumuamini Mungu lazima pia wawe watu wa amani.

Amesema kwa pamoja lazima waikatae chuki miongoni mwao, kulipiza kisasi na kufanya ghasia, hasa zile zinazofanywa kwa kutumia jina la dini au Mungu mwenyewe. Akiwahubiria watu waliofurika kwenye msikiti huo, Papa Francis amesema ziara yake ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, isingekuwa imekamilika iwapo asingekutana na jamii ya Waislamu.

Amesema Mungu ni amani, na hivyo amewasihi waumini wa Kikristo, Kiislamu na viongozi wa kimila kushirikiana kwa pamoja ili kuvimaliza vita vya nchini humo. Nchi hiyo imejikuta katika ghasia zinazochochewa kidini na kusababisha vifo vya maelfu ya watu, huku wengine wakiachwa bila makaazi, tangu mnamo mwaka 2013.

Wananchi wana matumaini na ziara ya Papa

Mmoja wa wakaazi wa Bangui, Alexandre Emede, aliyekuwa miongoni mwa watu waliojitokeza kumlaki Papa Francis, amesema ziara ya kiongozi huyo wa kidini itakuwa na manufaa kwa wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Papa Francis akisalimiana na wakaazi wa kambi ya watu wasio na makaazi, Bangui

Papa Francis akisalimiana na wakaazi wa kambi ya watu wasio na makaazi, Bangui

''Nina imani Papa Francis ametuletea amani. Tunamuomba kila mmoja, kila mwananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mkristo au Muislamu, kuanza kujisafisha ndani ya mioyo yao na kuwa na amani miongoni mwa kila mmoja, ili nchi yetu iweze kusonga mbele,'' alisema Emede.

Hapo jana Papa Francis mwenye umri wa miaka 78, alikutana na wawakilishi wa makanisa ya Kiinjili, ambapo alisema kukosekana kwa amani na umoja kati ya makanisa mbalimbali ni kashfa.

Aidha, Papa Francis amekutana na kiongozi wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-Panza, alizuru kambi ya watu wasio na makaazi na aliadhimisha Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Notre Dame, ambapo aliwatolea wito Wakristo kuwasamehe maadui zao ili kuondokana na ghasia.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amezuru katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, licha ya kuwepo wasiwasi kuhusu usalama wake. Ghasia kati ya wanamgambo wa Kikristo na Kiislamu, zilizuka mwezi Machi mwaka 2013, baada ya kundi la waasi wa Kiislamu la Seleka, kumpindua Rais Francois Bozize, aliyekuwa Mkristo.

Papa Francis leo anakamilisha ziara ya siku sita barani Afrika iliyomfikisha hadi kwenye nchi za Kenya na Uganda. Hiyo ni ziara ya kwanza kwa Papa Francis barani Afrika, na ya 11 katika maeneo mbalimbali duniani, tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, mwaka 2013.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com