1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
ImaniItaly

Papa Leo aadhimisha mwaka mmoja kwa kuwaombea viongozi

8 Mei 2026

Papa Leo XIV amewaombea viongozi wa ulimwengu ili Mungu awasaidie kusimamisha ghasia zinazoendelea na badala yake kujizatiti katika juhudi za kuleta amani, huku mvutano wa kimataifa ukiendelea kuongezeka.

https://p.dw.com/p/5DV0s
Vatikan 2026 | Papa Leo XIV. akiwa mbele ya hadhira katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Picha: Stefano Costantino/TTL/Avalon/Photoshot/picture alliance

Katika hotuba hiyo ya kuadhimishwa mwaka moja akiwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani katika mji wa kale wa Pompei wenye alama za mji ulioharibiwa enzi za utawala wa Warumi, Papa Leo wa XIV aliwaombea viongozi wa dunia.

Ametoa hotuba hiyo siku moja baada ya kukutana na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Marco Rubio katika makao makuu ya Vatican, kufuatia mvutano uliojitokeza baina ya Papa Leona Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu vita vya Iran, Israel na Marekani, ambavyo Papa alikuwa amevikosoa hadharani.

Papa Leo: Nyakati hazijabadilika

Alisema "Nyakati hazijabadilika. Vita bado vinaendelea katika sehemu nyingi za dunia, na hali hii inahitaji maamuzi mapya si kwa upande wa kiuchumi na kisiasa pekee bali pia kiroho na kidini. Hatuwezi kuzoea kutazama picha za vifo ambazo vyombo vya habari vinatuonyesha kila siku. Kutoka katika mahali hapa patakatifu, tunainua sala yetu kwa imani leo."

Katika mji huu wa Pompei ulioko kilomita 245 kutoka Vatican Papa Leo aliendesha misa katika siku maalum ya kumuenzi maarufu kama mama yetu wa Pompei sikukuu ambayo ilishabihiana na siku alipotawazwa kuwa Papa Leo

Sikukuu hiyo huadhimisha uwekaji wa jiwe la msingi la mahali patakatifu pa Bikira Maria wa Pompeii mwaka 1876. Usiku wa kuchaguliwa kwake, Papa Leo alimwomba Bikiria Maria na kuwaomba waumini waliokusanyika katika  kanisa la Mt. Petro waendelee kumwombea kwa ajili ya utume wake mpya pamoja na amani ya ulimwengu

Mahali Patakatifu ni nini hasa?

Mahali patakatifu panahusishwa kwa karibu na Bartolo Longo, ambaye awali alikuwa mshiriki wa imani ya ushetani kabla ya kuokoka na kujitolea maisha yake katika kazi za hisani kwa ajili ya mayatima, wafungwa na watu maskini. Kabla ya kifo chake, Papa Francis aliidhinisha muujiza uliokuwa muhimu kwa ajili ya kumtangaza Longo kuwa mtakatifu, na baadaye Papa Leo akamtangaza rasmi kuwa mtakatifu.

Akihutubia waumini Papa Leo alisema hii ni siku nzuri sana ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu alipochaguliwa: "Ni siku nzuri sana, iliyojaa baraka. Ninajihisi mwenye neema kubwa kwa kuweza kufika mahali hapa patakatifu.”

Katika ziara hiyo, Papa Leo alikutana na wagonjwa na watu wenye ulemavu wanaohudumiwa kwenye kituo cha huduma za kijamii kinachohusishwa na mahali hapo.

Wengi wavutiwa na unyenyekevu wa Papa Leo

Maelfu ya raia wa Italia walimkaribisha Papa Leo, wengi wakionesha kuvutiwa na unyenyekevu wake pamoja na utayari wake wa kuzungumzia masuala ya kijamii na kisiasa kwa uwazi. Baadhi walirejelea tofauti zake za hivi karibuni na Rais Donald Trump, wakisisitiza kuwa Papa amebakia sasa akilenga zaidi mahubiri ya neon la Mungu kuliko kuingia katika mivutano ya kisiasa.