1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Leo XIV aendeleza ujumbe wa Amani Cameroon

16 Aprili 2026

Papa Leo wa Kumi na Nne asafiri Bamenda kuhubiri amani katika eneo lililogubikwa na mgogoro wa kujitenga, akikutana na viongozi wa dini na waathirika wa machafuko.

https://p.dw.com/p/5CGhQ
Vatikan | Papa Leo XIV.
Papa Leo XIV atashiriki Misa maalum kwa wakazi wa Bamenda, mji ulioko karibu na mpaka wa Cameroon na Nigeria.Picha: Vatican Media/ZUMA Press/IMAGO

Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Leo wa Kumi na Nne, yuko safarini kuelekea jiji la Bamenda, magharibi mwa Cameroon, kuhubiri ujumbe wa amani katika eneo ambalo limekuwa kitovu cha mgogoro wa wanaharakati wanaotaka kujitenga, mgogoro ambao mashirika ya kibinadamu yameutaja kuwa miongoni mwa migogoro iliyopuuzwa zaidi duniani.

Papa Leo ataongoza mkutano wa amani unaowakutanisha viongozi wa dini mbalimbali, lengo ni kuangazia juhudi za pamoja za kidini katika kumaliza mgogoro huo na kuwasaidia waathirika waliopitia mateso.

Aidha, atashiriki Misa maalum kwa wakazi wa Bamenda, mji ulioko karibu na mpaka wa Cameroon na Nigeria.

Papa aliwasili nchini humo Jumatano, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya mataifa manne barani Afrika. Katika hotuba yake ya kuwasili, alisisitiza umuhimu wa kupambana na ufisadi na akazungumzia wajibu wa uongozi wa kisiasa.

Kabla ya ziara ya Papa, wapiganaji wa kujitenga walitangaza kusitisha mapigano kwa siku tatu, wakisema wanataka kuonyesha uwajibikaji na kuheshimu utu wa binadamu. Hata hivyo, licha ya kupungua kwa mashambulizi katika miaka ya karibuni, mazungumzo ya amani bado yamesimama na hakuna dalili ya suluhu ya kudumu.