1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Imani

Mwaka mmoja wa Papa Leo: Tunafahamu nini hadi sasa?

8 Mei 2026

Katika vyombo vya habari, ulimwengu unamjua Papa Leo, ambaye amesimama kama kiongozi wa Kanisa Katoliki kwa mwaka mmoja. Lakini mwanahistoria wa kanisa Jörg Ernesti haoni mtazamo ulio wazi.

https://p.dw.com/p/5DTEf
Vatikan 2025 | Papa Leo XIV. akisherehekea Misa ya Pentekoste katika Kanisa la Mtakatifu Petro
Papa Leo XIV atimiza mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuongoza Kanisa KatolikiPicha: Andrew Medichini/AP Photo/picture alliance

Kardinali Robert Prevost alipochaguliwa kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, alichagua kutambulika kama Papa Leo wa Kumi na Nne. Katika maadhimisho hayo, mwandishi wa Deutsche Welle, Christoph Strack, alifanya mahojiano maalum na mwanahistoria wa Kanisa Katoliki, Profesa Jörg Ernesti , kuhusu tathmini yake ya mwaka mmoja wa Papa Leo XIV kama kiongozi wa Kanisa hilo. 

Mei 8 mwaka 2025 Kardinali Robert Prevost alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki duniani. Kama ishara ya ya kuchaguliwa kwake, moshi mweupe wa kihistoria, unaofahamika kama Habemus Papam ulionekana ukifuka juu ya kanisa la Sistine ukiashiria kupatikana kwake.

Mwanahistoria wa Kanisa Katoliki, Profesa Jörg Ernesti wa Chuo Kikuu cha Augsburg kinachomshangaza zaidi kuhusu Papa Leo XIV ni namna anavyoongoza kwa utulivu mkubwa na busara. Hili linaonekana wazi hata kwa vyombo vya habari vya Italia ambavyo humtaja kama asiye na kauli za pupa na badala yake huchagua maneno aliyoyapima kwa kina.

Achagua kufuata njia ya mtangulizi wake

Profesa Ernesti anaeleza kuwa Papa Leo XIV amekuwa akisisitiza mara kwa mara mara mwendelezo na kufuata njia iliyowekwa na mtangulizi wake, Papa Francis. Kwa mujibu wa wachambuzi, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki hajabatilisha maamuzi muhimu ya mtangulizi wake , bali amejitahidi kuyaendeleza.

Miongoni mwa masuala machache aliyoyafanya tofauti na Papa Francis hadi sasa ni kuboresha ushirikiano na Sekretarieti ya serikali ya Vatican hasa katika masuala ya diplomasia na sera za kigeni.

Katika uwanja wa kimataifa, Papa Leo XIV ametoa umuhimu mkubwa kwa mabara ya Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.  Hivi karibuni alifanya ziara yake kubwa ya kwanza Afrika ambapo alizitembelea nchi nne za Algeria, Angola, Cameroon na Guinea ya Ikweta kwa takriban siku 11. Kulingana na Profesa Ernesti ni wazi kuwa Kanisa Katoliki linakua kwa upande wa Afrika kwa wastani wa asilimia 3 kila mwaka wakati kwa Ulaya haliongezeki.

Mvutano kati yake na Rais Donald Trump

Aidha Mwanahistoria huyo anabainisha kuwa ukweli kwamba Papa Leo anatoka Marekani unampa nafasi ya kipekee. Hivi karibuni kulipotokea mvutano kati yake na  Rais Donald Trump, alionesha msimamo wake wazi kuhusu masuala ya wahamiaji zikiwemo hatua za Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha ya Marekani ICE dhidi ya wahamiaji.

Vatikan 2026 | Papa Leo XIV. alipompokea Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio
Uhusiano kati ya Washington na Vatican umeingia doa kutokana na ukosoaji mkali uliotolewa na Rais Donald Trump dhidi ya Papa kutokana na miito yake juu ya vita vya nchini IranPicha: Simone Risoluti/Vatican Media/REUTERS

Tofauti hizo zilizidishwa pia na msimamo wa Papa Leo kuhusu vita vya Iran na suala la silaha za nyuklia. Katika mvutano huo hakujibizana kwa jazba na utawala wa Trump bali alisisitiza heshima ya taasisi ya upapa na kuzingatia maadili ya Kanisa.

Profesa Ernesti anasema hatua ya rais kumshambulia Papa hadharani ni jambo lisilo na mfano katika historia ya kisasa, lakini Papa Leo alijibu kwa hekima, akiacha kauli kali zitolewe zaidi kupitia Sekretarieti ya Vatican na wawakilishi wa Kanisa katika Umoja wa Mataifa.

Pamoja na hayo, kuna jambo moja ambalo bado hajalifanya linalosubiriwa kwa hamu kubwa: Waraka mkuu wa kwanza wa Papa kwa Kanisa. Kwa kawaida, waraka huo huonyesha mwelekeo wa kitheolojia wa utawala mzima wa Papa. Hadi sasa, Papa Leo hajaweka wazi dira hiyo, suala ambalo limewaacha wengi wakiwa na shauku ya kuusikia.