1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palestina yataka mazungumzo yaendelee

8 Agosti 2014

Licha ya kuanza tena kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, ujumbe wa Palestina kwenye mazungumzo ya amani mjini Cairo umesema mazungumzo ya kusaka amani ya kudumu yanaendelea.

https://p.dw.com/p/1CrWy
Mashambulizi ya Israel kwenya Ukanda wa Gaza tarehe 8 Agosti 2014.
Mashambulizi ya Israel kwenya Ukanda wa Gaza tarehe 8 Agosti 2014.Picha: Reuters

Mkuu wa ujumbe wa Palestina kwenye mazungumzo hayo yanayosimamiwa na serikali ya Misri, Azzam al-Ahmed, aliwaambia waandishi wa habari kwamba timu yake haitazamii kuondoka Cairo bila ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.

"Tumewaambia wapatanishi wa Misri kwamba tumekaa hapa ili tufikie makubaliano ya mwisho ambayo yatarejesha haki za Wapalestina," alisema al-Ahmed. Makundi ya Hamas na Islamic Jihad kwenye Ukanda wa Gaza, yalishasema kwamba hayakubaliani na kuendelea kusitishwa kwa mapigano, lakini yanataka mazungumzo ya Cairo yaendelee.

Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Misri imesema hivi leo (8 Agosti) kwamba hadi sasa tayari kulishakuwa na mambo kadhaa muhimu kwa Wapalestina, ambayo yalishafikiwa makubaliano, na kwamba yaliyosalia ni machache tu. Misri imetoa wito wa kusitishwa tena mapigano yaliyozuka alfajiri ya leo.

Israel yarusha makombora 10

Kwa mujibu wa maafisa wa Palestina, moja ya makombora 10 ya Israel lilitua kwenye msikiti na kumuua mvulana wa miaka 10 huko Gaza, huku majeruhi kadhaa wakipelekwa kwenye kwenye hospitali ya Shifa.

Roketi linalosemekana kurushwa na Hamas likielekea Israel.
Roketi linalosemekana kurushwa na Hamas likielekea Israel.Picha: picture-alliance/dpa

Polisi nchini Israel inasema watu wawili wamejeruhiwa leo, kufuatia maroketi yaliyorushwa na Hamas kusini mwa nchi hiyo. Waumini wa Kiislamu wameonekana mchana wa leo wakiswali Sala ya Ijumaa nje ya msikiti huo ulioharibiwa vibaya na mashambulizi ya Israel.

Watu waliokuwa wameanza kurejea kwenye mabaki ya nyumba zao, sasa wamekimbilia tena kwenye majengo ya Umoja wa Mataifa baada ya mashambulizi kuanza tena. Katika mtaa wa al-Tuffah, wakimbizi kadhaa wameonekana wakiwa wanaishi kwenye madarasa, nguo zikiwa zinaning´inia kwenye kingo za baraza, huku wengine wakijipanga foleni kungojea msaada wa chakula wa Umoja wa Mataifa.

Israel yawaondosha wajumbe wake Cairo

Ingawa haijawa wazi ikiwa kuzuka tena huku kwa mashambulizi kunamaanisha kuwa mazungumzo ya kusaka amani yameshindikana moja kwa moja, lakini taarifa zinasema tayari wajumbe wa Israel walishaondoka mjini Cairo, hata kabla ya muda rasmi wa kutisisha mapigano kwa muda haujamalizika asubuhi ya leo.

"Mazungumzo mjini Cairo yalijengwa juu ya sharti moja ambalo ni usitishaji wa aina zote za fujo usio masharti. Sasa Hamas ilipovunja makubaliano hayo, pale iliporusha maroketi kuelekea Israel, walivunja sharti hilo la mazungumzo na hakutakuwa na majadiliano vita vikimalizika," alisema msemaji wa serikali ya Israel, Mark Regev.

Kijana Abed Samara akiwa amejeruhiwa katika Ukanda wa Magharibi.
Kijana Abed Samara akiwa amejeruhiwa katika Ukanda wa Magharibi.Picha: DW/A. Samara

Pande zote mbili, Hamas na Israel, zinakabiliwa na shinikizo la kimataifa ili zifikie makubaliano, ingawa kila upande una masharti magumu kwa mwengine. Israel inataka Hamas inyang'anywe silaha au izuiwe kupata silaha nyengine, huku Hamas ikiitaka Israel iondowe mzingiro wake dhidi ya Gaza na mipaka yote ifunguliwe.

Mwezi mmoja wa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza umeshasababisha hadi sasa vifo vya takribani Wapalestina 1,900, wengi wao wakiwa raia wa kawaida, nayo Israel ikipoteza wanajeshi 64 na raia watatu. Umoja wa Mataifa unasema watoto 447 ni miongoni mwa Wapalestina waliouawa kwenye mashambulizi hayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf