1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Organization of the Petroleum Exporting Countries (OPEC)
Picha: RYAD KRAMDI/AFP/Getty Images
SiasaUjerumani

OPEC+ yaidhinisha hatua ya kupunguza uzalishaji wa mafuta

17 Oktoba 2022

Nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC+ zimekubaliana kwa pamoja kuidhinisha hatua ya kupunguza kiwango cha uzalishaji mafuta, licha ya Marekani kuikemea hatua hiyo na kusema imechochewa kisiasa.

https://p.dw.com/p/4IGRo

Hatua hiyo ya nchi wanachama wa OPEC+ imeidhinishwa rasmi jana licha ya onyo la Marekani. Washington imekuwa ikiishutumu Saudi Arabia kula njama na Urusi na kuyashinikiza mataifa mengine kuunga mkono hatua hiyo ambayo inasema itaongeza mapato ya kigeni ya Urusi na kupunguza makali ya vikwazo vya mataifa wa Magharibi dhidi ya Urusi.

Saudia hata hivyo imekanusha leo kuiunga mkono Urusi katika uvamizi wake nchini Ukraine, huku Waziri wa nishati wa jimbo la Ghuba Suhail al-Mazrouei akisema kuwa uamuzi wa OPEC+ ambao uliidhinishwa kwa kauli moja, ulikuwa wa kiufundi na usiyo na malengo yoyote ya kisiasa.

Soma zaidi:OPEC yapunguza ugavi huku kukiwa na hofu ya mfumuko wa bei 

Mfalme wa Saudia Salman bin Abdulaziz amesema Ufalme huo unawajibika kwa bidii ili kusaidia utulivu na usawa katika masoko ya mafuta, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kudumisha makubaliano ya muungano wa nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC+.

Wanamemba wa OPEC+ washikamana

Infografik Karte OPEC+ Mitgliedsstaaten DE
Ramani ya Mataifa ya OPEC+

Waziri wa ulinzi Mwanamfalme Khalid bin Salman, amesema kuwa uamuzi wa Oktoba 5 wa kupunguza uzalishaji wa mapipa milioni 2 kwa siku, ulichukuliwa licha ya masoko ya mafuta kuwa katika wakati mgumu, na kwamba uamuzi huo uliamuliwa kwa kauli moja na kwa kuzingatia masuala ya kiuchumi. Kauli yake iliungwa mkono na baadhi ya mawaziri wa OPEC+ wakiwemo wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Kuweit, Oman na Bahrain.

Soma zaidi: Biden aondoka Saudi Arabia baada ya kukamilisha ziara yake ya kwanza ya Mashariki ya Kati kama Rais

Akikutana jana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa OPEC Haitham Al Ghais, Waziri wa nishati wa Algeria Mohamed Arkab ameuita uamuzi huo kuwa "wa kihistoria": 

 

"Tulizungumza kuhusu masuala kadhaa yanayohusiana na sekta ya nishati nchini Algeria, njia za kuendeleza shughuli nchini Algeria, na usaidizi wa OPEC katika suala hili. Tulijadili pia soko la kimataifa la mafuta na uamuzi wa kihistoria wa hivi majuzi uliochukuliwa Vienna na ambao ungeleta usawa na utulivu katika masoko."

Uhusiano wa Marekani na Saudia

FILE PHOTO: Saudi Crown Prince Mohammed bin Salman and U.S. President Joe Biden meet at Al Salman Palace upon his arrival in Jeddah, Saudi Arabia
Rais wa Marekani Joe Biden (kushoto) akiwa na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman mjini Jeddah, Saudia ArabiaPicha: SAUDI ROYAL COURT/REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden amebaini kuwa uhusiano kati ya nchi yake na Saudia utaathirika kufuatia hatua hiyo ya OPEC+ kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa milioni 2 kwa siku, lakini kama watangulizi wake, atakabiliana na vikwazo endapo ataendelea kuvutana na nchi hiyo. Biden alilaumiwa nchini mwake baada ya kufanya ziara nchini Saudia mwezi Juni na kusalimiana na Mwanamfalme Mohammed bin Salman, licha ya kusema kuwa alikuwa akikiuka haki za binaadamu.

Soma zaidi: Biden kubadili mwelekeo wa mahusiano na Saudia

Maseneta kadhaa nchini Marekani wamehimiza nchi yao kusitisha uhusiano na Saudi Arabia ikiwemo mauzo ya silaha. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanahofia kuwa mvutano wa Biden na Saudia, unaweza kupelekea nchi hiyo kuzigeukia Urusi na China, lakini wataalamu wengine wana shaka kuwa Ufalme huo unaweza kufanya hivyo kwa urahisi baada ya miaka 80 ya ushirikiano na Marekani.