Olmert akutana na Abbas Jerusalem | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Olmert akutana na Abbas Jerusalem

Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas na waziri mkuu wa Israeli Ehud Olmert, leo wamekutana kuzungumzia masuala tete kuhusiana na utaifa wa Palestina. Mkutano huu ni mmoja kati ya mfululizo wa mazungumzo baina ya Olmert na Abbas kwa azma ya kuandaa mkutano mkubwa wa eneo zima unaotarajiwa kufanyika mwezi wa Novemba mwaka huu.

Nani atadhibiti mlima wa hekalu jijini Jerusalem?

Nani atadhibiti mlima wa hekalu jijini Jerusalem?

Kulingana na msemaji wa serikali ya Israel, Bw. David Baker, mkutano kati ya Ehud Olmert wa Israel na Mpalestina Mahmoud Abbas ulienda vizuri na mazungumzo yalikuwa wazi. Masuala yaliyozungumziwa ni ya msingi kuelekea kuwepo mataifa mawili kwa makabila mawili, alisema msemaji huyu. Afisa wa ngazi ya juu kutoka upande wa Palestina lakini alisema, masuala muhimu yalizungumziwa kwa ujumla tu.

Rais Abbas alitaka masuala ya mipaka na mustakabali wa wakimbizi wa Israel na Palestina yazingatiwe kwenye mazungumzo haya, lakini kama alivyosema mshauri wa Abbas aliyehudhuria mkutano na Ehud Olmert mazungumzo hayakuwa ya undani. Jana Abbas alionya kuwa mkutano wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika Novemba hautakuwa na maana yoyote ikiwa Israel itasisitiza juu ya matakwa yake. Abbas aliongeza anataka mazungumzo yawe ni mapana zaidi kuhusu makubaliano ya amani.

Pendekezo moja lililojadiliwa ni kuweka eneo la mlima wa hekalu kati kati mwa mji mkongwe wa Jerusalem, eneo ambalo ni takatifu kwa pande zote mbili, lidhibitiwe na dini hizi tatu zinazoamini Mungu mmoja. Haya aliyasema afisa mmoja wa serikali ya Israel akihojiwa na Redio Israel.

Waziri mkuu Ehud Olmert alimkaribisha Mahmoud Abbas kwenye nyumba yake rasmi mjini Jerusalem ambapo walizungumza kwa muda wa saa mbili. Mara iliyopita wiki tatu zilizopita walikutana mjini Jericho katika ukingo wa Mgharibi wa mto Jordan West Bank. Kabla ya mkutano mkubwa wa Novemba, viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana mara mbili au tatu nyingine.

Kulingana na wadadisi wa mambo ya kisiasa nchini Israel, Ehud Olmert, baada ya serikali yake kutokuwa na mafanikio mengi na kushindwa kwa jeshi lake kwenye vita dhidi ya Hamas nchini Lebanon, hana haraka kuendeleza mazungumzo haya na kufikia suluhisho la mwisho, akihofia baraza lake la mawaziri litaweza kugawanyika. Hadi sasa, serikali yake haijataja itakubali nini ili amani ipatikane.

Marekani inatumai mkutano wa eneo la Mashariki ya Kati hapo Novemba utafanikiwa kuutambua utaifa wa Palestina licha ya mgawanyiko miongoni mwa Wapalestina. Kundi la Hamas linalotawala eneo la ukanda wa Gaza lilipinga mazungumzo kati ya Olmert na Rais Abbas ambaye chama chake cha Fatah kinatawala kwenye eneo la Magharibi mwa mto Jordan. Hamas ilisema mkutano huu ni hatua nyingine ya kukitenganisha chama cha Hamas. Afisa mmoja wa Hamas, Bw. Sami Abu Zuhri, alisema mazungumzo hayatafikia popote wakati Israel inakataa kuheshimu haki za Wapalestina na kumaliza kuwakandamiza.

Suala lingine ambalo rais Abbas alilitaja katika mazungumzo na waziri mkuu Ehud Olmert ni juu ya hali ngumu ya usafiri kwa Wapalestina kwenye eneo la ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Kwa mujibu wa msemaji wake Baker, waziri mkuu Olmert alimuambia Abbas kuwa serikali hivi punde itaandaa mpango wa kuruhusu kusafiri kwa njia huru kati ya miji mikubwa.

 • Tarehe 28.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH8w
 • Tarehe 28.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH8w

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com