Obama na McCain wakubaliana kuhusu vikosi zaidi kuongezwa Irak na Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama na McCain wakubaliana kuhusu vikosi zaidi kuongezwa Irak na Afghanistan

Lakini watofautina kuhusu idadi

Seneta Barak Obama

Seneta Barak Obama

Wanaogombea kwenda Ikulu nchini Marekani kwa tiketi za vyama viwili vikuu nchini humo , Barak Obama wa chama cha Demokratic na mwenzake John McCain wa chama cha Republican wanajaribu kila mmoja kutoa mikakati ya kujipatia ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Baraka Obama ameweka bayana kile kinachoweza kuitwa mwelekeo wake wa sera za kigeni za Marekani ikiwa atachaguliwa kuwa rais.Suala muhimu ni kuhusu wanajeshi wake walioko Irak na Afghanistan.Amesema kuwa vikosi vya Marekani vitaondolewa Iraq katika mda wa miazi 16 akitoa sababu.

„Vita hivi vinatuzuia kujihami dhidi ya tisho lolote lile na kupoteza nafasi nyingi ambazo tungezipata. Vita hivi vinapunguza uwezo wetu wa kiusalama, msimamo wetu duniani, uwezo wetu kijeshi, uchumi wetu pamoja na nyenzo zinazohitajika kukabiliana na changamoto za karne ya 21. Kwa upande mwingine mwelekeo wetu pamoja na shabaha kuhusu Irak si mkakati sawa wa kuifanya Marekani kuwa salama."

Lakini mpinzani wake wa chama cha Republican, John McCain amejibu kwa kusema yeye, na wala sio mpinzani wake, anaejua jinsi ya kushinda.

La ajabu ni kuwa watu hao wawili jumanne ni kama waliungana kuhusu haja ya kuwa na vikosi zaidi ili kupambana dhidi ya Wataliban na wapiganaji wa Al Qaida nchini Afghanistan katika vita ambavyo Obama, akiwa mjini Washington alisema ni lazima wavishinde.

„Sasa ndio wakati muafaka wa kuongeza vikosi vyetu kuwashinikiza viongozi wa Iraq kuelekea suluhisho la kisiasa,na kujenga upya jeshi letu na kutathmini shabaha yetu kuhusu Afghanistn pamoja na suala zima la tisho la usalama wetu."

Wakati akijiandaa kufanya ziara ndefu barani Ulaya na Mashariki ya Kati , Obama amesema kuwa atatuma askari elf saba wa ziada nchini Afghanistan.Mwenzake McCain akasema kuwa wanajeshi wa ziada wanaohitajika ni zaidi ya elf 10.Aidha amemkemea Obama kwa kushindwa kueleza jinsi anavyopanga kutumia wanajeshi hao na pia kwa kupuuza mafanikio ya sasa ya Marekani nchini Iraq.

McCain akiwa Albuquerque,New Mexico,amesema kuwa Seneta Obama amekosea kwani ufanisi wa sasa wa vikosi vya Marekani nchini Irak na Afghanistan vitamuwezesha rais atakaefuata kurithi hali ya Iraq ambapo maadui wa Marekani watakuwa wanakimbia kujifcha.

McCain ameongeza kuwa Seneta Obama atawambia kuwa hatuwezi kushinda vita vya Afghanistan bila kushindwa nchini Irak.Yeye akasema kuwa vikosi zaidi vinahitajika Afghanistan,jambo ambalo liliulazimisha upande wa Obama kujibu kuwa amekopa msimamo wa mtu wao kwani hapo awali alikuwa amesema kuwa alikuwa anapinga kutumwa vikosi zaidi katika maeneo hayo.

Malumbano hayo yakiwa yanaendelea vigogo hao wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kushughulikia uchumi wa taifa hilo.Taarifa mpya kutoka huko zinaeleza kuwa uchumi wa Marekani unazidi kulegalega huku sarafu yake ya dola ikiwa inashuka kwa thamani ikilinganishwa na sarafu ya Euro.Kwa sasa Euro moja ni sawa na dola 1.60.

 • Tarehe 16.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EdSM
 • Tarehe 16.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EdSM
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com