Njama ya Al-Qaida kushambulia ndege yafichuliwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Njama ya Al-Qaida kushambulia ndege yafichuliwa

Marekani imesema imezuia njama za al Qaida kutaka kuiripua ndege ya abiria, kwa kutumia bomu linalofichwa kwenye nguo za ndani. Maafisa wanasema bomu hilo linafanana na lile lililojaribiwa na Al Qaida mwaka 2009.

Marekani yagundua njama za kuripua ndege

Marekani yagundua njama za kuripua ndege

Kwa mujibu wa taarifa kutoka serikali ya Marekani, njama hizo za kuripua ndege zilikuwa zikifanywa na tawoi la al Qaida nchini Yemen. Taarifa hizo zinasema kwamba njama hizo ziligunduliwa zikiwa bado katika hatua za mwanzo, na hakuna shirika lolote la ndege ambalo lilikuwa hatarini.

Afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba inaaminika al Qaida ilitaka kuilenga ndege ya abiria inayosafiri kwenda Marekani.

Al Qaida ilitaka kushambulia mwaka mmoja tangu alipouawa Osama bin Laden nchini Pakistan.

Al Qaida ilitaka kushambulia mwaka mmoja tangu alipouawa Osama bin Laden nchini Pakistan.

Lililenga maadhimisho ya kifo cha Osama bin Laden

Kuwepo kwa njama hizo na kuvunjwa kwake kulitangazwa siku moja baada ya kutimia mwaka mmoja tangu kiongozi wa mtandao wa al Qaida, Osama bin Laden kuuawa na kikosi maalum cha jeshi la Marekani. Mwenyekiti wa kamati ya bunge la Marekani inayoshughulikia masuala ya kijasusi, Dianne Feinstein, amelipongeza shirika la kijasusi la Marekani CIA, kuvunja kile alichokiita hila za al Qaida, ambazo zingeiripua ndege inayokwenda Marekani, kutumia aina mpya ya bomu ambalo ni vigumu kugunduliwa na mashine za upekuzi.

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Leon Panetta, amesema kuwepo kwa njama hiyo kunadhihirisha haja ya Marekani kuwa macho muda wote. ''Kitu ambacho kinadhihirishwa wazi na kisa hiki, ni kwamba nchi hii inapaswa kuendelea kuwa macho na kuchukua tahadhari dhidi ya wale wanaonuia kuidhuru. Tutachukua hatua zote zinazohitajika, kuhakikisha usalama wa Marekani''. Alisema Panetta.

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Leon Panetta.

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Leon Panetta.

Bomu lisilofichuliwa na vyombo vya ukaguzi

Shirika la upelelezi la Marekani, FBI, limesema kuwa bomu hilo lilikamatwa katika nchi ya kigeni, na ni aina moja na mabomu mengine yaliyotumiwa na al Qaida katika ghuba ya uarabuni, katika majaribio kadhaa ya kigaidi, yakiwemo yale dhidi ya ndege, na hata dhidi ya watu binafsi waliolengwa kuuawa. Kama mabomu mengine hayo, hili jipya nalo halikutengenezwa kwa metali, na hivyo lisingeweza kutambuliwa na vifaa kukagua silaha.

Hata hivyo, Afisa mmoja wa kupambana na ugaidi amesema kuwa al Qaida ilikuwa imelifanyia marekebisho bomu hili, ili lisishindwe kuripuka kama ilivyotokea mwaka 2009.

Naibu msemaji wa baraza la usalama la Marekani Caitlin Hayden, amesema kwamba Rais Barack Obama aliarifiwa kuhusu bomu hilo mwezi April, na kuhakikishiwa kuwa lisingeweza kusababisha kitisho kwa maisha ya watu.Amesema Rais Obama alitoa maagizo kwa idara ya usalama wa ndani ya nchi na mashirika ya kijasusi, kuhakikisha kuwa mashambulizi ya aina hiyo yanazuiwa.

Msemaji wa idara ya Usalama wa ndani Matt Chandler amesema kuwa kuwa jaribio hilo limeonyesha wazi azma ya maadui wao kuilenga sekta ya usafiri wa anga, na akaongezea kuwa wataendelea kutumia mbinu zote na teknolojia ya kisasa, kuhakikisha usalama wa ndege na viwanja vya ndege.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com