1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu: Israel itajiamulia masuala yake ya usalama

Amina Mjahid
17 Aprili 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewaambia mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na Uingereza, kwamba nchi yake ina haki ya kujilinda na itafikia maamuzi yake yenyewe linapokuja suala la usalama wake.

https://p.dw.com/p/4etLh
Baerbock akiwa Israel | Netanyahu
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana leo na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na mwenzake wa Uingereza David Cameron na kuwashukuru kwa kuiunga mkono nchi yake. Baada ya hilo akawambia kwa uwazi kabisa kwamba masuala ya usalama ya Israel yataamuliwa na nchi yenyewe huku akisisitiza kuwa wana haki ya kujilinda. 

David Cameron amesema anatumai jibu lolote litakalotoka Israel kwa Iran litatekelezwa kwa njia ambayo haitotanua mzozo uliopo.

Nae Annalena Baerbock amesema yeye ameweka wazi kabisa katika mazungumzo yake na Netanyahu pamoja na viongozi wengine nchini Israel kwamba, Kanda ya Mashariki ya Kati haipaswi kuburuzwa na kuingia katika hali ambayo matokeo yake hayatabiriki.

Israel yahimizwa kutojibu shambulizi la Iran

Huku hayo yakiarifiwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo kujadili hatua ya kuiongezea vikwazo Iran baada ya kuishambulia Israel siku ya Jumamosi. Viongozi wa Umoja huo ulio na nchi wanachama 27 wanakutana mjini Brussels wakati mataifa yaliyo na nguvu duniani yakiendelea na juhudi zao za kuzuwia mgogoro wa Mashariki ya Kati kutanuka ikiwa ni zaidi ya miezi sita tangu vilipoanza vita kati ya Israel na Hamas.

Israel haijasema ni vipi itakavyojibu shambulizi la Iran

Israel Netanjahu, Galant na Gantz wakiwa mjini Tel Aviv
Wanachama wa Baraza la mawaziri lenye jukumu la kusimamia vita Israel, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Ulinzi Yoav Galant na kiongozi wa zamani wa upinzani Benny GantzPicha: Abir Sultan via REUTERS

Israel hadi sasa haijasema ni vipi itakavyojibu shambulizi la Iran, lakini viongozi wa Ulaya wameiomba kujizuwiya huku wakisema wapo tayari kuiwekea Iran vikwazo zaidi kufuatia hatua yake hiyo. Mgogoro wa Mashariki ya kati pia unaendelea kujadiliwa kwa kina katika mkutano wa Mawaziri wa nchi za nje wa kundi la nchi tajiri kiviwanda la G7, wanaokutana kwa siku tatu mjini Capri Italia.

Wakati hayo yakijiri waziri wa mambo ya nchi za nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, amesema majadiliano kati ya Israel na Hamas ya kujaribu kuwaokoa mateka wanaoshikiliwa mjini Gaza yamekwama. Al Thani amesema wanajaribu kila njia ya kuyafufua mazungumzo hayo.

Israel: Mashambulizi ya Iran hayatapoteza lengo letu Gaza

Qatar Marekani na Misri kwa wiki kadhaa sasa, wamekuwa wakijaribu kutafuta njia ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita mjini Gaza na kuachiwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas, ili Israel nayo iwaachie wafungwa wa kipalestina inaowashikilia.

Vita kati ya Israel na Hamas vilianza wakati kundi hilo la wanamgambo liliposhambulia kusini kwa Israel nakusababisha mauaji ya Waisraeli 1,200 na baadae Israel ikaanzisha mashambulizi dhidi ya kundi hilo katika Ukanda wa Gaza ambayo hadi sasa yamesababisha mauaji ya zaidi ya watu 33,899 kulingana na wizara ya afya ya Hamas.

Baerbock ziarani Israel tena kusaka suluhisho la mgogoro

afp/ap/reuters