Netanyahu aonyesha mshikamano na wananchi wa Iran
5 Januari 2026
Akizungumza mwanzoni mwa kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri mjini Jerusalem, Netanyahu amesema Israel inasimama pamoja na mapambano ya wananchi wa Iran na matarajio yao ya uhuru, haki na demokrasia.
Kauli ya Waziri Mkuu huyo ameitoa wakati maandamano makubwa yanaendelea kushuhudiwa nchini Iran, ambapo raia wamekuwa wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi.
Katika maelezo yake, Netanyahu pia amesema huenda dunia ikashuhudia wakati ambao wananchi wa Iran wanachukua kile alichokiita hatma yao mikononi mwao.
Mwaka uliopita, Israel iliingia kwenye mzozo na Iran uliodumu kwa muda wa siku 12, na kwa ushirikiano na Marekani ilifanya mashambulizi yaliyolenga baadhi ya vituo muhimu vya nyuklia vya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Israel imeendelea kuushutumu uongozi wa Tehran kwa kile inachodai ni mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia, jambo inaloliona kuwa tishio kwa usalama wake.