1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za kivita zashambulia Yemen

6 Mei 2015

Ndege za kivita za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia zimefanya zaidi ya mashambulizi 30 usiku wa kuamkia leo, kaskazini-magharibi mwa Yemen kwenye majimbo ya Saada na Hajja, mpakani na Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/1FKlk
Moja ya ndege zilizoharibiwa kufuatia mashambulizi ya angani yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya uwanja wa ndege wa Sana'a.
Moja ya ndege zilizoharibiwa kufuatia mashambulizi ya angani yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya uwanja wa ndege wa Sana'a.Picha: Reuters/K. Abdullah

Maafisa wa Yemen wamesema mashambulizi hayo ya anga yamefanywa kwenye mji wa mpakani wa Najran ulio umbali wa kilomita tatu kutoka kwenye mpaka wa Yemen, baada ya waasi wa Houthi nchini Yemen kurusha makombora na roketi jana, yaliyoharibu shule moja ya wasichana na hospitali.

Hilo ni shambulizi la kwanza kufanywa na waasi hao katika eneo la Saudi Arabia, tangu muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulipoanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya waasi hao Machi 26, mwaka huu. Kwa mujibu wa maafisa hao, mashambulizi hayo ya makombora yalikuwa yakifanywa kutoka kwenye mpaka wa Saudi Arabia.

Waasi wa Houthi
Waasi wa HouthiPicha: picture-alliance/AP Photo

Eneo la Saada ni ngome muhimu kwa waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran. Duru za waasi hao zimeeleza kuwa raia 43 wameuawa na wengine wapatao 100 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ambayo yamefanyika hadi leo alfajiri. Hata hivyo idadi hiyo bado haijathibitishwa.

Wakati huo huo, Rais Francois Hollande wa Ufaransa, amesema anaunga mkono juhudi za operesheni hizo katika kuhakikisha Yemen inakuwa na utulivu. Rais Hollande alikuwa akihudhuria mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano wa mataifa ya Ghuba-GCC, mjini Riyadh, akiwa ni kiongozi wa kwanza wa nchi za Magharibi kuhudhuria mkutano wa baraza hilo.

Rais Francois Hollande
Rais Francois HollandePicha: Reuters/G. Fuentes

Akizungumza jana wakati akiufungua mkutano huo, Rais Hollande amesema Ufaransa haitasita kuchukua hatua yoyote ile, hata ya kijeshi kwa ajili ya washirika wake. Kauli hiyo ameitoa siku moja baada ya Ufaransa kusaini mkataba wa euro bilioni 6.3 wa kuipatia Qatar, ndege 24 za kivita.

Mashirika ya misaada yaelezea wasiwasi wao

Wakati hayo yakijiri, mashirika 22 ya misaada yanayofanya kazi nchini Yemen, yameonya kuwa msaada wao unaweza ukamalizika, iwapo njia za ardhini, majini na anga hazitofunguliwa ili kuruhusu mafuta yaingizwe nchini humo.

Mkurugenzi mkaazi wa shirika la kimataifa la misaada la Save the Children, Edward Santiago, amesema maisha ya mamilioni ya watu yako hatarini na hasa watoto na hali ikiendelea kuwa hivyo, basi watashindwa kuendelea na shughuli za kutoa misaada ya kibinaadamu.

Naye msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu utoaji wa misaada ya Kibinaadamu-OCHA, Jens Laerke, amesema muungano wa jeshi hilo, unaulenga uwanja wa ndege wa Sanaa, hivyo njia za ndege zimeharibika na ndege haziwezi kutua.

Msemaji wa OCHA, Jens Laerke
Msemaji wa OCHA, Jens LaerkePicha: cc-by-nc-nd/United Nations Geneva, Jean-Marc Ferré

''Hili ni janga, na uwanja huu ni njia pekee ya kuingizia misaada ya kibinaadamu nchini, ambako maelfu ya watu wanahitaji haraka msaada wa kuyaokoa maisha yao,'' alisema Laerke.

Ama kwa upande mwingine, kiongozi wa kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran, Sheikh Hassan Nasrallah, amesema operesheni ya kijeshi inayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi, imeshindwa kufikia malengo yake.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE
Mhariri: Gakuba Daniel