1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanajeshi wa zamani Esper aapishwa kuiongoza Pentagon

Sylvia Mwehozi
24 Julai 2019

Mwanajeshi mkongwe, Mark Esper ameapishwa kuwa waziri mpya wa ulinzi wa Marekani, saa chache baada ya kuidhinishwa na bunge na kuhitimisha kipindi kirefu cha wizara hiyo ya Pentagon bila ya kuwa kiongozi rasmi. 

https://p.dw.com/p/3MeMa
USA Mark Esper soll neuer Verteidigunsminister werden
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Esper aliapishwa katika Ikulu ya White House na jaji wa Mahakama Kuu, Samuel Alito katika hafla iliyohudhuriwa na Rais Donald Trump pamoja na wabunge kadhaa wa Republican. Aliidhinishwa na bunge la Marekani kwa kura 90-8 saa chache kabla.

Esper mwenye miaka 55 na mwanajeshi mkongwe ambaye alikuwa mshawishi katika kampuni ya kutengeneza silaha ya Raytheon, alipigiwa kura nyingi na vyama vyote licha ya hapo awali seneta mmoja wa Democrats Elizabeth Warren kuhoji juu ya mahusiano yake na kampuni hiyo. Katika hafla hiyo rais Trump hakusita kummwagia sifa Esper.

''Nina uhakika atakuwa waziri bora wa ulinzi, sina shaka kuhusu hilo. Yeye ni bora katika kila nyanja na tunafurahi kwa kujiunga nasi,'' alisema Trump.

Pentagon haikuwa na waziri kamili tangu Jim Mattis alipojiuzulu mwezi Desemba kutokana na tofauti za kisera na Trump. Wanachama wote wa bunge kutoka vyama vyote walimtaka rais kujaza nafasi hiyo kwa haraka. Awali, Trump alikuwa amempendekeza mkurugenzi wa zamani wa kampuni ya Boeing Patrick Shanahan, lakini aliliondoa jina lake baada ya kubainika alikumbwa na tuhuma za ukatili wa kijinsia ndani ya familia yake.

USA Designierter Verteidiungsminister Mark Asper  bei seiner Anhörung im Senat
Esper akihojiwa mbele ya kamati ya bunge ya silahaPicha: picture-alliance/MediaPunch/CNP/S. Reynolds

Esper mwanajeshi wa zamani alihudumu kama msaidizi wa bunge na afisa wa wizara ya ulinzi chini ya utawala wa rais wa Republican George W. Bush kabla ya kufanya kazi na kampuni ya Raytheon. Amekuwa mkuu wa jeshi tangu Novemba 2017. Esper ambaye ana uzoefu mpana katika masuala ya ulinzi, amesema anakusudia kuendeleza sera za utawala wa Trump za kuimarisha utayari wa jeshi, kukuza ushirikiano wa kiusalama duniani na kuleta mageuzi ndani ya Pentagon.

''Asante sana kwa uongozi wako na uwajibikaji thabiti katika ulinzi wa taifa na kwa washirika wetu wote wa jeshi. Jeshi letu limepata mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni, asante kwa uongozi wako na tuko tayari kukabiliana na changamoto yoyote itakayojitokeza.'

Kura nne kati ya nane za kumpinga Esper zilitoka kwa maseneta wa Democrats wanaotafuta kuwania urais wa mwaka 2020.

Vyanzo: AP/Reuters