Museveni akiri dosari za kiufundi kwenye uchaguzi Uganda
15 Januari 2026
Raia nchini Uganda wamepiga kura Alhamisi katika zoezi hilo lililogubikwa na dosari kadhaa zikiwemo za kiufundi na kuchelewa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura. Dosari hizo zimelaleamikiwa pia na Yoweri Museveni anayekitetea kiti chake katika uchaguzi huo.
Mapema Alhamisi, raia wa Uganda walifika vituoni kupiga kura ili kumchagua rais na wabunge wakati vituo vya kupigia kura vikichelewa kufunguliwa kwa kipindi cha hadi saa nne. Sababu kubwa inatajwa kuwa ni matatizo ya kiufundi.
Museveni anayekitetea kiti chake amethibitisha kuwa amekabiliana pia na changamoto hizo alipokwenda katika kituo chake cha kupigia kura akisema kuwa, "Waganda kote duniani wanasikiliza nilichofanya hapa. Mimi ni mimi ni mfano mzuri. Niliweka alama ya kidole gumba cha kulia, mashine haikukikubali. Niliweka cha kushoto kwangu, haikukubali. Kwa nini? Inawezekana kwamba tulipoichukua tulitumia pande tofauti. Lakini mwsho wa siku kilichoamua kilikuwa uso. Mashine ilikubali kuusoma uso. Kwa hivyo mashine inafanya kazi."
Museveni amesema aliarifiwa kuhusu dosari hizo na amedai kuwa aliunga mkono pendekezo la tume ya uchaguzi la kupiga kura kwa njia ya kawaida badala ya kidijitali kwani haikuwa sahihi kwa watu kurejea makwao bila kupiga kura. Ameagiza pia uchunguzi ufanyike ili kubaini sababu za mashine hizo kushindwa kufanya kazi.
Kyagulani alalamikia hujuma za uchaguzi
Mpinzani wa Museveni, Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine mara baada ya kupiga kura iameishutumu serikali kwa kuyajaza masanduku ya kura na kuzima huduma ya intaneti.
Kyagulani amesema, "Hatutarajii uchaguzi huru na wa haki. Tume ya uchaguzi haihusiki na uchaguzi huu. Jeshi ndilo linalouendesha. Tunavyoongea sasa hivi intaneti imezimwa na wanachama wetu 750 wako jela. Tunavyoongea hapa utekaji nyara hata kwa mawakala wetu wa kuhesabu kura unaendelea. Lakini tunategemea nguvu ya watu wa Uganda kuwa watasimama imara na kudhihirisha nia yao."
Ulinzi mkali umeshuhudiwa katika maeneo mengi nchini humo huku polisi wakionya kuwa, shughuli hiyo ya uchaguzi haihalalishi kufanyika kwa vitendo vya uhalifu.
Kulingana na shirika la habari la AFP waandishi wa habari wamekuwa wakinyanyaswa. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights watch limelaani vikali hatua ya serikali ya Uganda ya kusitisha shughuli za mashirika takriban 10 ya kiraia yakiwemo yanayofuatilia uchaguzi.
Katika uchaguzi huo Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, anapambania kuendeleza utawala wake kwa muhula mwingine, huku wachambuzi wakisema anaendelea kutegemea kwa kiasi kikubwa vyombo vya ulinzi kudumisha mamlaka yake.