Motsepe: AFCON itachezwa Morocco kama ilivyopangwa
7 Oktoba 2025
Kauli hii ni licha ya maandamano ya kila siku dhidi ya serikali ambayo yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya wiki moja.
Vijana wa Morocco wamekuwa wakiandamana kwa siku kadhaa mfululizo wakitaka kukomeshwa kwa ufisadi na mabadiliko ya serikali. Wanadai maboresho ya huduma za kijamii, hasa afya na elimu, na walionyesha hasira kuhusu ukosefu wa usawa wa kijamii.
Miongoni mwa waandamanaji waliojitokeza haya ni baadhi ya maoni yao:
"Tumejitokeza kwa ajili ya watu, si kwa ajili ya vijana tu. Kwa ajili ya kila mtu. Ndugu zetu wa kiume na wa kike walio wadogo lazima waweze kunufaika na elimu bora. Wazee lazima waweze kupata hospitali nzuri. Hatupingi nchi wala ujenzi wa viwanja vya michezo au majumba ya opera. Tunataka kujivunia mafanikio kama hayo, tunataka pia kujivunia hospitali zetu na vyuo vikuu vyetu.”
"Tunadai haki zetu za elimu na huduma za afya. Hizi ni haki, si mapendeleo. Hatuna haja na viwanja vya michezo. Na ukiangalia wakazi wa Haouz [eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi mwaka 2023] ambao bado hawajapokea chochote, lakini uwanja wa michezo umejengwa na kukamilika haraka... Katika kijiji changu, karibu na Taroudant, hatuna hospitali wala duka la dawa.”
Ratiba ya mechi
Maandamano haya yanajiri huku taifa hilo la hilo la Afrika Kaskazini likitarajia kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Afrika kuanzia Disemba 21 hadi Januari 18 mwaka huu, ikijumuisha timu za kitaifa 24.
Wachezaji nyota kama Mohamed Salah wa Misri na Liverpool, pamoja na Achraf Hakimi wa Morocco na Paris Saint-Germain wanatarajiwa kushiriki.
Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa soka Afrika uliofanyika Kinshasa, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, alisema:
"Tunayo imani kubwa kwamba AFCON itafanyika kama ilivyopangwa. Morocco ni mpango A, mpango B na mpango C.”
Aliongeza kuwa CAF itashirikiana na serikali na wananchi wa Morocco kuhakikisha AFCON ya kihistoria.
Morocco iliwahi kuwa mwenyeji wa AFCON mwaka 1988 wakati huo mashindano hayo yalijumuisha timu 8 tu na ilijiondoa kama mwenyeji wa toleo la 2015 kutokana na hofu ya virusi vya Ebola.
Motsepe alieleza kuwa CAF ina matumaini ya kufufua Ligi ya Soka Afrika, ambayo ilizinduliwa kwa shangwe lakini ikasitishwa mwaka 2023 baada ya toleo moja. Badala ya timu 24 na mechi 14 kila moja, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilishinda toleo lililopunguzwa la timu 8.
Motsepe alirithi uongozi wa CAF ikiwa na madeni makubwa kutoka kwa Ahmed Ahmed mwaka 2021, baada ya kupigwa marufuku na FIFA kwa kukiuka kanuni za uaminifu, matumizi mabaya ya madaraka na ufujaji wa fedha. Lakini tangu wakati huo, hali ya kifedha imeimarika.