1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMorocco

Maandamano Morocco kushinikiza mageuzi katika sekta ya afya

3 Oktoba 2025

Maandamano mapya ya kudai mageuzi katika sekta za afya na elimu yamefanyika nchini Morocco kwa siku ya sita mfululizo, kufuatia vifo vya watu watatu vilivyotokea wakati wa makabiliano yaliyotokea jana usiku.

https://p.dw.com/p/51RKz
Morocco Rabat 2025 | Maafisa wa usalama washika doria
Maafisa wa usalama wakishika doria kuzuia maandamano ya kudai mageuzi katika sekta ya elimu na afya mjini Rabat, MoroccoPicha: Ahmed El Jechtimi/REUTERS

Mjini Rabat, waandamanaji waliobeba bendera za taifa walikusanyika barabarani na kushinikiza kuimarishwa kwa sekta ya afya badala ya kupewa kipaumbele kwa ujenzi wa viwanja vya michezo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP, maandamano ya siku ya Alhamisi yalifanyika kwa amani bila kuripotiwa visa vya vurugu.

Maandamano mengine pia yameripotiwa katika miji ya Casablanca, Marrakech, na Agadir, yote yakifanyika kwa utulivu.

Hali hiyo ya kuongezeka kwa maandamano imechochewa na hasira ya umma kuhusu ukosefu wa usawa wa kijamii, hasa baada ya ripoti za mwezi uliopita kuhusu vifo vya wanawake wanne wajawazito katika hospitali ya umma mjini Agadir—tukio lililoibua maswali kuhusu ubora wa huduma za afya nchini humo.

Wengi wa waandamanaji wanaamini kuwa sekta za afya na elimu ya umma zinahitaji maboresho ya haraka, hasa wakati ambapo mamlaka zinaendelea kusukuma miradi mikubwa ya miundombinu kwa ajili ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi ujao, pamoja na Kombe la Dunia la FIFA la mwaka 2030.